Lugha, Fasihi na Elimu

Ni kinaya Kenya kuandaa Siku ya Kiswahili Duniani bila Baraza la lugha hiyo!

June 12th, 2024 1 min read

NA BITUGI MATUNDURA

MNAMO Julai 7, 2024, ulimwengu utaadhimisha makala ya tatu ya Siku ya Kiswahili Duniani (SIKIDU).

Hafla hiyo imekuwa ikiadhimishwa tangu mwaka 2022, kufuatia tangazo la Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) lililoteua tarehe hiyo kwenye kikao chake cha 41 jijini Paris, Ufaransa mwaka 2021.

Tofauti na maadhimisho ya nyuma ya siku hiyo, ambapo Kenya ilitapatapa kwa kukosa utaratibu mwafaka, hafla ya mwaka 2024 yamkini itakuwa na upekee kwa sababu tatu.

Kwanza, Kenya ndio mwenyeji wa tamasha hiyo ya siku tatu, itakayoanza Julai 5, 2024.

Pili, Serikali imekwisha kuzindua kamati itakayoratibu maadhimisho hayo. Kamati hiyo inashirikiana na Wizara ya Masuala ya Jinsia, Utamaduni na Turathi za Kitaifa, inayoongozwa na Waziri Aisha Jumwa.

Tatu, Serikali imetenga fedha kufadhili maadhimisho hayo yatakayohusisha wajumbe wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki – ambao wamealikwa kukongamana nchini.

Hata hivyo, inasikitisha mno kwamba, Kenya bado haijaunda Baraza la Kiswahili (BAKIKE).

Mataifa mengine ya jumuiya kama vile Tanzania yana asasi hiyo, huku Uganda ikipiga hatua za kuridhisha katika kuunda chombo hicho.

Pindi litakapoundwa, Baraza la Kiswahili la Taifa la Kenya litatwikwa majukumu mbalimbali yakiwemo: kutoa ushauri rasmi kwa Serikali pamoja na kushirikisha na kuratibu masuala yote kuhusu ukuzaji na uendelezaji wa matumizi ya Kiswahili kama lugha ya taifa na lugha rasmi.

Kiswahili ni lugha muhimu ya Kiafrika katika ulingo wa kimataifa. Inazungumzwa na takriban watu milioni 200.