Dimba

Manchester United yamthamini Kobbie Mainoo kwa kuifungia bao la ushindi FA

June 1st, 2024 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

SI ajabu kuwa thamani ya Kobbie Mainoo imepanda zaidi ya mara 60 kutoka Sh112.4 milioni (Yuro 800,000) mnamo Juni 20, 2023, hadi Sh7 bilioni (Euro 50 milioni) mnamo Mei 27, 2024.

Katika kipindi cha miezi miwili na wiki mbili zilizopita, Mainoo ameongeza thamani yake sokoni kwa Sh2.1 bilioni (Euro 15 milioni).

Kupanda kwa thamani hiyo kunatokana na uchezaji wa hali ya juu ambao tineja huyo ameonyesha kambini mwa Manchester United msimu huu 2023-2024 uliokamilika majuzi.

Licha ya United kusikitisha kwenye Ligi Kuu (EPL) ikimaliza ligi nambari nane, pamoja na kubanduliwa Kombe la Carabao na Klabu Bingwa Ulaya (Uefa) mapema, mmojawapo wa wachezaji waliofana uwanjani Old Trafford ni Mainoo.

Kazi yake ilishuhudia kocha Erik ten Hag akimpa mechi 35 msimu huu uliotamatika, zikiwemo 24 katika EPL na sita Kombe la FA.

Katika mechi tatu za ligi alifunga goli; United wakipepeta Wolves 4-3, wakafinya Newcastle 3-2 na kusare 2-2 na mahasimu Liverpool.

Alifunga pia katika Kombe la FA; ushindi dhidi ya Newport County 4-2 katika raundi ya nne na dhidi ya majirani Manchester City 2-1 wakishinda fainali ya kombe hilo wikendi iliyopita.

Soma Pia: Manchester United yanyanyua taji la 13 FA, moja nyuma ya Arsenal

Inamaanisha kuwa mbali na majukumu ya kiungo mkabaji anayotekeleza, tineja huyu mwenye umri wa miaka 19 pia si mchache kufunga goli ukimpa nafasi.

Mabeki wa zamani wa United, Wes Morgan na Rio Ferdinand, wamelinganisha mchezo wa Mainoo na ule wa Mholanzi Clarence Seedorf.

Baadhi pia wanaamini anaonyesha sifa za Mfaransa Paul Pogba.

Majagina hao watatu waling’ara enzi zao kambini mwa Red Devils naye Seedorf akafanya makubwa akiwa kwa vigogo wa Italia, AC Milan, na wa Uhispania, Real Madrid.

Kumaanisha kuwa anafanya kazi nzuri kustahili sifa hizo, ingawa muda utakuwa msema kweli kama atafikia viwango vyao.

Mainoo alianza soka akiwa na umri wa miaka minne katika akademia ya Cheadle & Gatley kabla kiujiunga na Man United miaka mitano baadaye.

Kimataifa, hajachezea timu yoyote ya taifa ya watu wazima. Yeye ni mzaliwa na raia wa Uingereza mwenye asili ya Ghana.

Hata hivyo, Ghana imechelewa kutafuta huduma zake kwani Uingereza imemwita katika kikosi kinachojiandaa kwa Kombe la Ulaya (Euro) 2024 litakalofanyika nchini Ujerumani kuanzia Juni 14 hadi Julai 14.