Michezo

Manchester United yanyanyua taji la 13 FA, moja nyuma ya Arsenal

May 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

KLABU ya Manchester United imepunguza mwanya wa mataji ya Kombe la FA kati yake na mahasimu Arsenal baada ya kuivua ubingwa Manchester City kwa kuichapa 2-1 kwenye fainali ya Kombe la FA ugani Wembley, Jumamosi jioni.

United, ambayo itashiriki Europa baada ya ushindi huo muhimu, ina mataji 13 ya dimba hili, moja nyuma ya Arsenal inayoshikilia rekodi.

Ililipiza kisasi dhidi ya City kupitia mabao ya chipukizi Alejandro Garnacho na Kobbie Mainoo.

City, ilibwaga United 2-1 katika fainali mwaka 2023, na katika fainali ya Jumamosi, wachezaji wake walipoteza nafasi nzuri.

Phil Foden na Erling Haaland walipoteza nafasi za wazi.

Kocha Erik ten Hag amekuwa akikabiliwa na presha ya kufukuzwa kwa sababu ya msimu duni ambapo United ilimaliza Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika nafasi ya nane.

Josko Gvardiol alitunuku United zawadi ya bao la kwanza alipomchenga kipa wake Stefan Ortega akimrudishia mpira kupitia kichwa na kumpa Garnacho kazi rahisi ya kujaza bao katika wavu mtupu.

Mainoo kisha alikamilisha pasi safi kutoka kwa nahodha Bruno Fernandes ndani ya kisanduku kabla ya mapumziko. Mainoo sasa ni tineja wa kwanza Muingereza kufunga bao katika fainali ya Kombe la FA tangu Steve MacKenzie aliyefungia City dhidi ya Tottenham mwaka 1981.

Mashetani Wekundu wa United sasa wamelemea City mara sita katika mechi nane za FA wamekutana.