Habari za Kitaifa

Polisi walivyochana mbuga vitoa machozi vilipowaishia mbele ya waandamanaji

Na FRIDAH OKACHI June 27th, 2024 2 min read

MAAFISA wa polisi waliokuwa wanalinda afisi za Mbunge wa Dagoretti Kusini John ‘KJ’ Kiarie walilazimika kutorokea usalama wao Jumanne, wakati vitoa machozi walivyokuwa wakirushia waandamanaji kuisha.

Wahalifu waliodai kuwa waandamanaji usiku wa Jumanne, Juni 25, 2024 walimfuata mbunge huyo baada ya kupiga kura ya “ndio’’ kwa Mswada wa Fedha 2024 licha ya kuandika barua ndefu ya kuomba msamaha kwa wapiga kura wake.

Wakati wa maandamano hayo, polisi mmoja wa kitengo cha AP alipoteza kidole kimoja.

Waandamanaji hao walisema afisi hiyo imekuwa ikiendeleza ufisadi wakati wa kutoa basari kwa wakazi.

Mlinzi wa afisi hiyo Bw Isaac Khaemba, alisema waliotekeleza kitendo hicho ni waandamanaji zaidi ya 1,000 walivuja ukuta ili kupata nafasi ya kuingia.

“Mchana maandamano yalikuwa na utulivu sana. Saa kumi jioni walirudi hapa na kubomoa ukuta ambao umezingira afisi hii. Wakati huo, polisi walitumia vitoa machozi kuwatawanya,” alisimulia Bw Khaemba jinsi hali ilianza.

“Baadaye walikuja kwenye afisi hiyo na kuamuru wanunuliwe maji ya kupangusa gesi ya kutoa machozi na mfanyakazi mwenza akawapa na kuenda,” alisema Bw Khaemba.

Baadhi ya vijana kwenye eneo la mkasa wakibomoa siku ya Jumatato| PICHA | FRIDAH OKACHI

Waandamanaji wapya walifika katika afisi hiyo mwendo wa saa mbili usiku na kuanza kurusha mawe. Maafisa wa polisi waliingilia kati hadi wakati vitoa machozi viliisha.

“Vitoa machozi viliisha, niliokolewa na polisi kutoka kituo cha Kabete. Polisi walitoroka na kuniacha kwenye lango na waandamanaji hao walianza kuchoma choo na kisha kuelekea katika afisi ya mbunge na kuchoma kila kitu,” alisema Bw Khaemba.

Waandamanaji hao walitoka katika eneo hilo baada ya kuhakikisha afisi hiyo imeteketea.

Msimamizi wa kituo cha polisi Bi Sarah Kimsar alithibitisha kuwa mmoja wa maafisa kutoka kituo chake alipoteza kidole wakati wa makabiliano makali na waandamanaji.

Baadhi ya karatasi za cheki zilizosalia | PICHA | FRIDAH OKACHI

“Wakazi hao ambao walikuwa wanaandamana, walikuwa wakirusha mawe. Mmoja wa maafisa wangu alipoteza kidole kwa njia ambayo haieleweki. Sasa hivi yuko hospitalini anapokea matibabu,” alisema Bi Kimsar.

Bi Kimsar, amewaomba wakazi wa Dagoretti Kusini kufanya maandamano ya amani bila kuharibu mali ya umma.

“Sheria inakubali kila mmoja kuwa na haki ya kufanya maandamano lakini isiwe ni maandamano ya kuharibu mali ya watu na umma.  Sasa hivi mbunge wa eneo hilo atahitaji kutumia pesa ambazo zingesaidia umma kujenga afisi hii upya,” alikamilisha Bi Kimsar.