Habari za Kitaifa

Raila awinda kura za AUC Afrika Magharibi huku vijana wakiandaa ‘siku saba za uasi’ Kenya

Na JUSTUS OCHIENG June 24th, 2024 2 min read

WAZIRI Mkuu wa zamani Raila Odinga sasa analenga kura za mataifa ya Magharibi mwa Nchi kupitia muungano wao wa kiuchumi, ECOWAS huku akitarajiwa atawasilisha rasmi nia yake ya kuwania Uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) wiki hii.

Mkuu wa kitengo cha mikakati katika kampeni za Bw Odinga, Balozi wa zamani wa Amerika Elkana Odembo, Jumapili alisema waziri huyo mkuu wa zamani alikutana na Rais wa Nigeria Bola Ahmed Tinubu wiki jana.

Wawili hao walikutana katika hafla ya kuapishwa kwa Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ambapo Raila alishauriana na Marais wengine na kuahidiwa uungwaji mkono pamoja na nafasi ya kuuza azma yake nchini mwao.

Serikali inatarajiwa wiki hii kuwasilisha stakabadhi za kiongozi huyo wa ODM kwa AU, hatua hiyo ikimpisha kuanza rasmi kampeni zake kwa wadhifa huo.

Uchaguzi wa AUC utaandaliwa Februari 2025.

Bw Odembo jana alisema Rais Tinubu alimhakikishia Raila uungwaji mkono wake na akamtaka amtembelee Nigeria kwa mashauriano na mazungumzo zaidi.

“Akiwa Afrika Kusini Raila aliandaa mazungumzo na Marais Denis Sassou Nguesso (Congo Brazzaville), Felix Tshisekedi (Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo), Samia Suluhu (Tanzania), Bola Tinubu (Nigeria) na Joao Laurenco (Angola),”

“Wote waliahidi kumuunga mkono na wakampa mwaliko awatembelee. Ualishi huu ni muhimu ikizingatiwa kuwa Nguesso anaongoza muungano wa kiuchumi wa mataifa yanayozungumza Kifaransa naye Tinubu ana ushawishi mkubwa ECOWAS,” Bw Odembo akaeleza Taifa Leo.

Kaika kiny’an’anyiro cha uenyekiti wa AUC, wapinzani wa Bw Odinga ambao wamejitokeza ni Makamu wa Rais wa Ushelisheli Vincent Meriton, Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Djibouti Mahmoud Youssouf na waziri wa zamani wa nchi za kigeni kutoka Somalia Fawzia Yusuf.

Bw Youssouf anasemekana kuwa kifua mbele katika nchi zinazongumza Kifaransa na Bw Odinga analenga kumtoa kijasho kupata uungwaji mkono wa baadhi ya mataifa hayo.

Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi ambaye pia ni waziri wa masuala ya kigeni, alikuwa ametangaza kuwa Kenya itawasilisha rasmi azma ya Bw Odinga kwa AU mnamo Juni 30 ambayo ni wiki hii.

Wiki mbili zilizopita, azma ya Raila ilipata uungwaji mkono kutoka kwa Zambia na Malawi ambazo ni nchi wanachama wa Muungano wa Kiuchumi wa Mataifa ya Kusini mwa Afrika (SADC).