Habari za Kitaifa

Rais aonya Wakenya dhidi ya ukabila akihimza umoja wa nchi

June 1st, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto amewahimiza Wakenya kudumisha umoja na uzalendo na wajiepushe na siasa za kikabila.

Akiongea katika uwanja wa michezo wa Masinde Muliro, Bungoma wakati wa hafla ya Madaraka Dei, Rais pia alikariri kuwa Kenya haitaendeleza siasa za kulenga watu binafsi na kuwatenga wananchi wengine.

Dkt Ruto alisema ajenda yake imejikita katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kote nchini bila kuzingatia jinsi watu walivyopiga kura katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

“Ninataka kuwahakikishia Wakenya kwamba hatutarejelea siasa za kikabila na zisizojumuisha watu wote, waliotupigia kura na wale ambao hawakutupigia kura,” akasema Rais Ruto.

Kiongozi wa taifa pia alitoa onyo kali kwa maafisa wa serikali wenye hulka ya kuiba au kuharibu mali ya umma.

“Maafisa wote wa serikali, kuanzia mimi, tutawajibishwa kwa matumizi ya rasilimali chini ya usimamizi wetu,” Rais Ruto akasema.

Aidha, aliwataka wale walionyakua ardhi za umma katika Kaunti ya Bungoma kuzisalimisha ili kutoa nafasi kwa upanuzi wa miradi kama Uwanja wa Masinde Muliro miongoni mwa miradi mingine yenye manufaa kwa umma.

Rais Ruto alitumia sherehe hizo za 61 tangu Kenya ilipopata madaraka ya kujitawala, kuorodhesha mafanikio ya serikali yake katika sekta ya kilimo.

Aidha, aliahidi kuwa serikali itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali katika pembe zote za nchi.

Maudhui ya sherehe za mwaka 2024 ni “Kilimo na Utoshelevu wa Chakula kwa Wote”.

Kwingineko, Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru, ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Magavana, alipinga vikali hatua yoyote inayoweza kuendeleza ukabila.

“Tulikuwa katika hali sawa ni hiyo katika mwaka wa 2007. Kama kiongozi wa Mlima Kenya siwezi kuruhusu watu wetu washawishiwe kujitenga na Wakenya wenzao,” akasema Bi Waiguru akiwa Kirinyaga.

Rais Ruto alisema serikali ya Kenya Kwanza itaendelea kuwekeza katika mipango ya miradi ya kupiga jeki sekta ya kilimo ili kuhakikisha kuwa taifa la Kenya linazalisha chakula cha kutosha kukidhi mahitaji ya raia.

“Sekta ya Kilimo huchangia asilimia 25 ya Jumla ya Utajiri wa Kitaifa (GDP). Aidha, hupiga jeki nguzo nyingine za maendeleo kama vile sekta ya utengenezaji bidhaa inayochangia asilimia 27 ya utajiri wa nchi,” Rais Ruto akaeleza.