Siasa

Ruto asalia kimya UDA wakikabana koo

May 30th, 2024 2 min read

CHARLES WASONGA NA BENSON MATHEKA

MZOZO unaendelea kutokota ndani ya chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA), kinachoongozwa na Rais William Ruto, viongozi wakionekana kutozungumza kwa sauti moja.

Hii ni baada ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Cleophas Malala kutishia kuwachukulia hatua za kinadhamu baadhi ya viongozi aliodai wanawakosea heshima Dkt Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua.

Huku misukosuko hiyo ikiendelea, kiongozi wa chama, Rais William Ruto hajasema lolote, hasa baada ya Wabunge kumshambulia naibu wake hadharani.

Kwenya taarifa, Bw Malala aliwashambulia wabunge Gathoni Wamuchomba (Githunguri), Oscar Sudi (Kapseret) na Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga akisema mienendo yao ya kuhujumu uongozi wa chama hicho haitavumiliwa.

Bw Sudi ni miongoni mwa viongozi chipukizi wa Kenya Kwanza ambao wamekuwa wakimshambulia Bw Gachagua huku Wamuchomba na Kahiga wakimtetea naibu rais.

“Hii iwe ni onyo kwenu. Mkomeshe vitendo na matamshi yetu yanayokiuka sheria na uongozi wa chama mlichoapa kuhudumia. Mkiendeleza mwenendo huu, chama kitachukua hatua za kinidhamu dhidi yenu,” Bw Malala akasema.

Juzi, Gavana Kahiga alifoka akimtaka Rais Ruto kuwadhibiti wandani wake kutoka eneo la Bonde la Ufa aliodai ni miongoni mwa wanasiasa wanaopiga vita Bw Gachagua.

“Aidha, ningependa kusema hapa mbele ya kila mtu kwamba, hatutaruhusu mtu wetu (Gachagua) kupitia yale ambayo Ruto alipitia mikononi mwa Uhuru Kenyatta. Hatutaruhusu mwana wetu adhulumiwe. Ndio maana tunamkata Rais awakomeshe baadhi ya watu wake wanaoendesha njama hii,” Gavana Kahiga akasema Jumapili iliyopita alipoandamana na Bw Gachagua kwa ibada katika eneo bunge la Kesses, Kaunti ya Uasin Gishu.

Baada ya siku hiyo, Bw Sudi alimkaripia Bw Gachagua kwa kumuonya yeye na wabunge wengine kutoka Bonde la Ufa dhidi ya kuingilia siasa za eneo la Mlima Kenya.

Mbunge huyo, ambaye ni mwandani wa karibu wa Rais Ruto, alisema Naibu Rais hana mamlaka ya kuelekeza mwanasiasa yeyote mahala pa kuendeshea siasa.

“Hauwezi kudhibiti ziara zangu. Ikiwa sote tungesalia katika maeneo bunge yetu, basi hatungekuwa serikalini. Ilitubidi kuzunguka kote nchini kuwashawishi Wakenya waupigie kura utawala huu,” Sudi akasema.

“Nitaendelea kukutana na watu hata katika eneo la Mlima Kenya huku nikiongoza mikutano ya harambee. Nilijifunza haya kutoka kwa rais mwenyewe na sitakoma,” akaongeza.

Naye Bi Wamuchomba amekuwa akipinga na kukosoa sera, maamuzi na misimamo mbalimbali ya serikali ya Rais Ruto licha ya kwamba, alidhaminiwa bungeni na chama cha UDA.

Ni kauli na misimamo kama hii iliyochangia Katibu Mkuu Bw Malala kuwaonya viongozi hao dhidi ya kuhujumu uongozi wa chama hicho na serikali iliyoko mamlakani.

Bw Malala pia aliwaonya mawaziri Moses Kuria (Utumishi wa Umma) na Kipchumba Murkomen (Barabara na Uchukuzi) dhidi ya kujihusisha na siasa, akisema kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

“Ewe Moses Kuria, Waziri Utumishi wa Umma, wajibu wako ni kuwahudumia wananchi kulingana na majukumu ya wizara yako. Ikiwa unataka kujiingiza katika siasa, unakaribishwa kujiuzulu na ujitose sawasawa katika ulingo wa siasa,” Bw Malala akasema.

Aidha, alimshauri Bw Murkomen hivi: “Vile vile, kama Waziri wa Barabara na Uchukuzi elekeza juhudi zako katika masuala mazito yanayokumba wizara yako kama ukarabati wa barabara zilizoharibiwa na mafuriko. Wahudumie Wakenya au ang’atuke na urejelee siasa.”

Jana, Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja alijiunga na wanaomshambulia Bw Gachagua akidai naibu rais anampiga vita mkubwa wake Rais Ruto.

Bw Sakaja anayemezea mate kiti cha mwenyekiti wa UDA kaunti ya Nairobi katika uchaguzi ujao wa chama alimtaka Bw Gachagua amheshimu Rais na viongozi wengine waliochaguliwa.

Gavana huyo alidai kuwa, kwa miaka miwili iliyopita, Bw Gachagua amekuwa akiwatisha viongozi wengine na hafai kulalamika akikosolewa.