Habari za Kitaifa

Serikali yasema haitaweza kuajiri walimu 46,000 wa JSS baada ya mswada wa fedha kuangushwa

Na WINNIE ATIENO June 29th, 2024 1 min read

SERIKALI haitaweza kuajiri walimu 46,000 wa Sekondari Msingi kwa Mkataba wa Kudumu kwa kukosa pesa baada ya Rais William Ruto kukataa kutia saini Mswada wa Fedha 2024.

Serikali ilikuwa imetenga pesa za kuwaajiri walimu hao katika bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2024/2025 ambayo ingefanikishwa kupitia Mswada huo.

“Hata hivyo, bajeti ilikataliwa na sasa ni lazima tuangalie vipaumbele. Watu wanapaswa kuelewa shida yetu kwa sababu pesa zinatokana na mapato tunayokusanya kutoka kwa walipa kodi. Suala la bajeti litaathiri uajiri wa walimu kwa kazi ya kudumu na ya pensheni,” Waziri la Elimu Ezekiel Machogu ambaye alizungumza wakati wa kufunga kongamano la Wakuu wa Shule za Sekondari Kenya, mjini Mombasa.

Mwezi uliopita, maelfu ya walimu wa JSS waliokuwa kwenye mgomo tangu Aprili 17, 2024, walirudi kazini hadi Julai 5, 2024 wakisubiri bajeti isomwe.

Awali Alhamisi, Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) Nancy Macharia alikuwa ametangazia walimu wa JSS ambao walifutwa kazi kwa kushiriki mgomo kwamba wanaweza kutuma maombi ili waweze kufutiwa kesi zao na kuajiriwa tena.

SOMA HAPA: Kung’ata na kupuliza: Serikali kuajiri tena walimu wa JSS waliofutwa kwa kugoma