Habari

Ushindi kwa Ruto wabunge wakimvukishia kwa urahisi Mswada tata wa Fedha


RAIS William Ruto ameandikisha ushindi wa kwanza baada ya wabunge 204 kuvukisha Mswada tata wa Fedha wa 2024 dhidi ya wabunge 115 walioupinga.

Shughuli hiyo ilijiri Alhamisi jioni baada ya wabunge kukamilisha mjadala kuhusu mswada huo ambao umechochea maandamano ya vijana kote nchini wakiupinga kwa kupendekeza ushuru utakaochangia kupanda kwa gharama ya maisha.

“Matokeo ya upigaji kura ni kama yafuatayo; wabunge 204 wamepiga kura ya NDIO huku 115 wakipiga kura ya LA,” akasema Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula.

“Suala la Mswada wa Fedha sasa limekamilishwa. Tusubiri kamati ya bunge lote, wabunge wenye mapendekezo ya marekebisho wayawasilishe kwa Karani wa Bunge na maafisa wake watayaandaa,” akaongeza.

Hatua hiyo sasa inaashiria kuwa Jumanne wiki ijayo marekebisho yaliyopendekezwa kufanyiwa mswada huo yatajadiliwa na kupigiwa kura.

Nyingi ya marekebisho hayo yalipendekezwa na Kamati ya Bunge kuhusu Fedha kwenye ripoti yake baada ya kuendesha vikao vya kukusanya maoni kuhusu mswada huo.

Miongoni mwa marekebisho hayo ni kuondolewa kwa ushuru wa VAT wa asimilia 16 kwa mkate, mafuta ya kupikia na kuongezwa kwa ushuru kwa huduma za kifedha.

Aidha, Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Molo Kuria Kimani ilipendekeza kuondoa ushuru wa magari wa asilimia 2.5, ushuru wa mazingira kwa bidhaa zinazotengenezwa nchini miongoni mwa ushuru zingine.