Akili Mali

Uzalishaji mbegu zinazostahimili athari za tabianchi 


KATIKA soko la Kiusyani, Kaunti Ndogo ya Kitui Mashinani, Kitui ndiko Muungano wa Kijamii wa Inyamandu unaendeleza shughuli zake za utengenezaji mbegu. 

Kitui ikiwa mojawapo ya kaunti zilizoorodheshwa kuwa miongoni mwa maeneo jangwa na nusu-jangwa (ASAL), Inyamandu CBO Seed Merchant inajituma kuunda mbegu za ndengu, kunde na mahindi.

Aidha, kupitia wakulima wake, huzalisha mbegu ambazo zinastahimili mikumbo ya mabadiliko ya tabianchi kama vile kiangazi, mafuriko na wadudu na magonjwa ya mimea.

Isitoshe, ni mbegu zinazotoa mazao kwa wingi.

Mkurugenzi Mkuu Inyamandu CBO Seed Merchant, John Kimanthi akionyesha ndengu ambazo muungano huo ulioko Kitui umezalisha. PICHA|SAMMY WAWERU

“Kabla kuingia sokoni, mbegu tunazounda hukaguliwa na kuidhinishwa na Taasisi ya Mbegu na Ustawishaji wa Mimea (Kephis),” anasema John Kimanthi, Mkurugenzi Mkuu wa Muungano huo.

Inyamandu CBO Seed Merchant ina kandarasi na wakulima wa nafaka, Kimanthi akifichua kwamba mwaka uliopita, 2023, walihudumu na idadi ya wakulima wasiopungua 100.

Huku muungano huo ukitengeneza mbegu zinazohimili athari za tabianchi, Kephis hukagua mimea ikiwa ingali shambani na baadaye sampuli za mbegu kabla kupelekwa kwenye kiwanda.

Muungano huo uliosajiliwa rasmi na Kephis, una kiwanda cha shughuli hiyo katika Soko la Kiusyani.

Shughuli za kupakia mbegu za nafaka zilizoundwa na Inyamandu CBO Seed Merchant Kitui, zikiendelea katika kiwanda chake. PICHA|SAMMY WAWERU

Kina mtambo wa kudondoa maganda, hasa ya kunde na ndengu.

“Vilevile, tuna mashine ya kuchanganya mbegu na dawa dhidi ya wadudu na magonjwa,” Kimanthi akaambia Akilimali Dijitali wakati wa mahojiano katika kiwanda cha muungano huo.

Huhudumu kwa karibu na Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo Kenya (Kalro), ambalo huwasambazia mbegu zilizoafikia vigezo faafu za kuzalisha.

Muungano huo ulianzishwa 2009 ukiwa na lengo la kusaidia wasiojiweza katika jamii kwa kuwapa chakula na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi.

Mbegu za kunde zilizotengezwa na Inyamandu CBO Seed Merchant Kitui. PICHA|SAMMY WAWERU

Isitoshe, ulikuwa unaendeleza kilimo cha ndengu na kukuza nyanya na mboga kwenye vivungulio (Greenhouse).

Miaka 15 baadaye, una kila sababu ya kutabasamu kutokana na mchango wake mkubwa katika sekta ya kilimo hasa kufuatia utengenezaji wa mbegu zinazostahimili athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kutoka uzalishaji wa tani 2 kwa mwaka za ndengu, Kimanthi, Mkurugenzi Mkuu anadokeza kwamba kwa sasa wametinga zaidi ya tani 9.

Kunde, muungano huo unazalisha wastani wa tani 4.5.

Ni kutokana na jitihada zake, United States Agency for International Development (USAID) kupitia mradi wake, Kenya Crops and Dairy Market Systems (KCDMS), uliokamilika 2023, muungano huo ulipata ufadhili kunogesha huduma.


John Kimanthi, Mkurugenzi Mkuu Inyamandu CBO Seed Merchant Kitui akielezea jinsi mbegu za nafaka huchanganywa na dawa dhidi ya wadudu na magonjwa. PICHA|SAMMY WAWERU