Habari Mseto

Vijana wadai msaidizi wa Wamboka alitekwa kufuatia bosi wake kupiga kura ya ‘La’

Na JESSE CHENGE June 27th, 2024 1 min read

MAANDAMANO katika mji wa Bungoma yaliendelea Alhamisi, huku mamia ya vijana wakilalamikia kutekwa kwa msaidizi binafsi wa Mbunge wa Bumula, Jack Wamboka, Wangila Wabomba.

Chini ya uongozi wa Ken Mupalia na Ignatius Nyukuri, vijana hao walisema tangu Jumanne, msaidizi wa Mbunge hajapatikana.

Msaidizi huyo alikuwa miongoni mwa waandamanaji jijini Nairobi dhidi ya mswada wa fedha alipopotea.

Vijana wenye hasira walimpa Inspekta Jenerali wa Polisi saa 24 kumwachilia Bw Wabomba mara moja.

“Wangila alikuwa tu anatekeleza haki yake ya kidemokrasia, kwa nini kumteka?” waliuliza.

Nyukuri alisema vijana ndio walioweka serikali ya William Ruto madarakani na akajiuliza kwa nini wamegeuka dhidi yao.

Walidai kwamba Wangila alitekwa kwa sababu tu mbunge wake alipiga kura dhidi ya mswada wa kodi ya juu.

Walitishia kulemaza biashara mjini Ijumaa iwapo hataachiliwa huru.

Awali, Bw Wamboka alisema alitembelea vituo vyote vya polisi, hospitali na mochari lakini hakumpata.

Alisema ikiwa serikali inawalenga wabunge waliopinga basi ‘wamchukue yeye’.

“Waje kwangu badala ya kwenda kwa msaidizi wangu ikiwa wanataka kutufunga midomo,” alisema Bw Wamboka.