Makala

Vitabu vya fasihi vilivyotia mori vijana wa Gen Z kupigania haki barabarani

Na OSCAR KAKAI June 28th, 2024 3 min read

RIWAYA ya mwandishi George Orwell ya “Shamba la Wanyama,” na mchezo wa dhihaka wa muigizaji na mwandishi maaufu kutoka Ukraine, Nicolai Gogol wa kitabu cha “The Government Inspector,” ni vitabu ambavyo vilichangia mapinduzi na kupigania haki dhidi ya serikali ya Urusi ya Czar.

Vitabu hivyo vimejaa sarakasi za makosa, kuonyesha dhihaka za uchoyo wa binadamu na ufisadi wa wanasiasa katika nchi ya Urusi suala ambalo lilichangia migomo shuleni.

Nchini Kenya, mori wa Gen Z dhidi ya Mswada wa Fedha 2024 kuhusu kile wanasema ni kunyanyaswa kwa kuongezwa kwa ushuru kunaaminika kusukumwa na vitabu vya tamthilia wanavyosoma shuleni.

Kulingana na walimu wa fahisi, riwaya hizo na hadithi fupi zenye maudhui kuhusu haki, kupambana na maisha kwa jamii, demokrasia, uongozi mbaya, ufisadi, kutelekezwa na viongozi, kutokujali, usaliti, umaskini, kukosa ajira, kukosa matumaini, matumizi mbaya ya mamlaka ya ofisi, ubadhirifu wa fedha, uchoyo, kujipiga kifua, ubinafsi, kazi ya vyombo vya habari, uongozi mbaya, ukabila, urafiki, ubeberu, haki ya kuongea na hisia mbaya imewapa nguvu vijana kutetea haki zao kwa jamii.

Baadhi ya vitabu hivyo ambavyo vimetajwa ni The Samaritan chake John Lara, Fathers of Nation chake Paul B Vitta, Parliament Owls chake Adipo Sidang, An Enemy of the People chake Henrik Ibsen, Betrayal in the City chake Francis Imbuga, Kigogo chake Pauline Kea, Tumbo Lisiloshiba chake Said Ahmed, Mstahiki Meya chake Timothy Arege, Kifo Kisimani chake Kithaka wa Mberia, Kidagaa Kimemwozea chake Ken Walibora na vingine ambavyo vimekuwa kwa miaka michache iliyopita.

Bw David Olengo, mwalimu wa lugha katika Shule ya Upili ya Kamito katika Kaunti ya Pokot Magharibi anasema kuwa riwaya hizo zimechangia Gen Z kupigania demokrasia na kupinga uongozi mbaya na ufisadi nchini.

“Vitabu hivyo vimewafanya Gen Z kupinga Mswada wa Fedha wa 2024. Roho ya mapinduizi ya vijana imechochewa na vitabu hivyo ambavyo tumekuwa tukifunza wanafunzi. Inaonekana serikali na maafisa wa uchunguzi hawajakuwa chonjo. Kile ambacho kiko kwenye vitabu hivyo ndio yamefanyika kwa wiki moja iliyopita,” anaeleza Bw Olengo.

Bw Olengo anasema kuwa vijana wanatumia apu na teknolojia ambayo huwaleta pamoja kutatua madhila yao.

“Vijana wamekuja na ubunifu. Siku hizi hatufundishi wanafunzi kupata alama ya A, tunawafunza kupata ujuzi ambao utawasaidia kuishi vyema katika jamii na jinsi uongozi hufanywa. Kwa mfano, kwenye kitabu cha The Samaritan kuhusu suala la dokezo la Biblia linahusu vijana kupigania haki dhidi ya maovu,” alifichua Bw Olengo.

Bw Olengo ambaye pia ni mwalimu wa michezo ya kuigiza anataja kuwa vijana wanatumia michezo ya kuingiza na nyimbo kuelezea kutoridhishwa kwao na serikali pamoja na viongozi.

“Wanatumia kufoka, neno la kutamka na mashairi kukejeli watu na serikali,” anasema.

Anasema kuwa maovu ambayo hutekelezwa na vingozi ama wanasiasa husambazwa kwenye mitandao ya kijamii kutumia maneno, video na picha.

Anasema kuwa vijana wanaelewa kuwa wale ambao walikuwa wakipigania haki wamesalitiwa na serikali.

“Watu kama Raila Odinga ambao wamekuwa wakipigania demokrasia wamesalitiwa na ndio sababu vijana wamesimama kupigania haki zao,” anasema.

Mamlaka ambayo hayapingwi

Bw Olengo anasema kuwa vitabu hivyo vinaelezea athari za mamlaka ambayo hayapigwi msasa na uchoyo.

“Wanaelewa kuhusu masuala ya kukamata serikali, manispaa na kaunti. Vitabu hivyo vinaelezea kuhusu viongozi ambao sio waaminifu na hawako karibu na raia na hawana usaidizi kwao. Dhuluma, ufisaidi wa wabunge huzima sauti za wanyonge. Hata hivyo, dhuluma hizo huchangia uasi kati ya wale hudhulumiwa wakiongozwa kama wacheza mchezo kwenye kitabu Parliament of Owls kama Iron Lady Owl na kusaidiwa na ndege wengine kuleta mabadiliko,” anasema Bw Olengo.

Bw Wycliffe Magero, mwalimu mkuu katika Shule ya Upili ya St Paul Kachibora katika Kaunti ya Trans-Nzoia anasema kuwa vitabu vya tamthilia ambavyo vinatumika shuleni vinahusu masuala ya jamii.

“Kizazi cha kisasa kimepata habari na kinaelewa haki zao. Wanapigania na msukumo wao hauhusu wanasiasa fulani bali haki zao. Hawafuati viongozi gizani kama sisi rika la miaka ya 70 na 80 ambapo tulikuwa tukifuata viongozi kama Kenneth Matiba ama Raila Odinga,” anasema.

Anasema kuwa wengi wa vijana wa Gen Z ni watoto wa watu wenye mapato ya kadiri na wanaelewa jinsi wazazi wao wamedhulumiwa na serikali.

“Ni watoto wa wafanyakazi wa serikali. Wakati wanaandaa maandamano hawana wasiwasi sababu wanajua watapata chakula wakirudi nyumbani. Mapinduzi hufanywa na watu wa mapato ya kadiri. Kwa muda mrefu watu wa mapato ya kadiri kama walimu wamekuwa wakilaumiwa kwa kutoshiriki kwenye uongozi lakini sasa watoto wetu wamechukua usukani,” anasema.

Bw Magero ambaye anaunga mkono Gen Z anasema kuwa wengi wao walienda shule za kibinafsi ambapo wanafunzwa kuhusu haki zao.

“Baada ya masomo ya shule ya upili wanajiunga na vyuo vikuu vya kibinafsi kama United States International University ((USIU),” anasema.

Anasema kuwa wengi wao wanaelewa jinsi serikali huendeshwa.

“Uongozi wa nchi ulisahau kuwa vitabu vya tamthilia sio tu kupita mtihani,” analeza.

Anasema kuwa Gen Z wanaelewa kuwa wako na uwezo wa kupata mawakili wazuri na familia zao zinajiweza.

“Wao huwa mbele kwenye maandamano sababu wanaungwa mkono na wazazi wao. Wako na uwezo wa kujua maisha yao na ukiwa uongozini utapata shida nao. Wale walishiriki kwenye maandamano ni watoto wa mawaziri, magavana na watu mashuhuri. Vladimir Lenin, mwana mapinduzi, mwanasiasa wa Urusi na mwanzilishi wa muungano wa Usovieti na kiongozi wa chama cha Bolshevik aliyetetea ujamaa na ukomunisti alikuwa mwana wa mtu wa mapato ya kadiri, mshona cherehani wa haiba ya juu Nikolai Vassilievich Ulyanov,” anaongeza Bw Magero.

[email protected]