Habari za Kitaifa

Wabunge walazimika kuzima simu kuhepa maelfu ya jumbe za Gen Z


WABUNGE walilazimika kuzima simu zao baada ya Wakenya kuwasiliana nao na kuwatumia jumbe kwa wingi kuwakashifu kwa kuunga mkono Mswada wa Fedha 2024 ambao raia wengi wanapinga.

Haya yalijiri baada ya nambari zao za simu kuchapishwa hadharani katika kampeni ya kuwashinikiza wakatae kupitisha mswada huo tata.

Wale waliopiga kura kuunga usomwe kwa mara ya pili Alhamisi ndio walikuwa na wakati mgumu wakitumiwa jumbe na raia waliojawa na hasira.

Vijana ambao hawakuridhika waliwasiliana na wabunge wa maeneo yao kuwakumbusha wakatae mswada huo.

“Simu zilikuwa nyingi, betri ya simu ilichukua dakika 15 kuisha moto. Tatizo kuu lilikuwa ukosefu wa maudhui hata kama mtu angeamua kuzungumza nao,” alisema kiranja wa wengi bungeni Silvanus Osoro.

Jumbe nyingi zilizotumiwa wabunge zilikuwa za kuwatishia kuwa hawatachaguliwa tena kwa kuunga mswada huo.

“Ukipitisha mswada huu, sahau kuchaguliwa tena,” ulisema ujumbe uliotumiwa mbunge mmoja.

Nambari nyingi za simu za wabunge zinazojulikana hadharani zimezimwa. Katika jitihada za kuthibitisha uhalisi wa nambari zilizosambazwa, Wabunge walitumiwa pesa nyingi kupitia Mpesa.

“Watu wengi walikuwa wakinitumia kiasi kidogo cha pesa, wakati mwingine kidogo kama shilingi mmoja, uwezekano wa kuthibitisha kama nambari ni yangu. Wengine waliomba niwatumie pesa,” Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa aliambia Taifa Leo.

“Nilipokea karibu Sh125,000, ambazo zilinifanya kutambua kuwa nina mashabiki huko nje. Baadhi ya watu waliuliza kwa nini nilipiga kura ya ‘ndiyo’ na walionyesha kusikitishwa. Lakini nilipowauliza waeleze mswada huo hawakuuelewa.”

Hali ilizidi kuwa mbaya huku baadhi ya watu wakitishia kufichua maisha ya kibinafsi ya wabunge hao na vitendo viovu.

Vitisho hivi vimezidisha wasiwasi miongoni mwa wabunge hao, huku wengine wakionyesha hofu kuhusu usalama wao na wa familia zao.

Katika bunge, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah alitoa malalamishi bungeni kuhusu kunyanyaswa na baadhi ya Wakenya.

Kunyanyaswa na baadhi ya Wakenya

Bw Ichung’wah alilalamika kwamba nambari zao za simu zimesambazwa kwenye mitandao ya kijamii, hivyo kuwalazimu kuzizima. Pia alisema wabunge walilazimika kuzima baadhi ya mitandao ya kijamii kutokana na hali hiyo.

“Najua wengi wa wabunge hawa nikiwemo mimi mwenyewe tumekumbana na unyanyasaji mwingi. Nilimuuliza kiongozi wa wachache kama naye aliteseka hivyo akaniambia hali yake ilikuwa mbaya zaidi. Wengi wa Wabunge hawa huwezi kuwapata kwenye simu zao kwa sababu wamefunga simu zao ikiwemo WhatsApp,” alisema Mbunge huyo wa Kikuyu.

Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya alisema vijana wamekata tamaa na wanatamani kusikilizwa, akifichua kuwa alipokea jumbe kadhaa kutoka kwa wapiga kura wa eneobunge lake.

“Sauti zao ni muhimu kwani wao ni sehemu ya ukombozi. Nilipokea jumbe chache za vitisho, ambazo zinaangazia jinsi vijana wamepoteza matumaini na wanahitaji kusikilizwa,” Mbunge Salasya alisema.

“Sauti zao ni muhimu katika harakati za ukombozi. Wengi hata walinitumia pesa kidogo, hata Sh1, ambazo kwa jumula zilifika Sh40,000,” mbunge huyo aliongeza.

Lakini Mbunge wa kuteuliwa John Mbadi alisema alipokea jumbe tatu pekee: mbili kwenye laini yake ya simu anayotumia sana na moja kwenye laini yake ya upili.

“Wakati wengine walipokea jumbe za chuki, jumbe zangu zilihusu tu kunisihi kushiriki katika mchakato wa kupiga kura, bila maudhui yoyote ya kuudhi,” alieleza.

Kwa Mbunge wa Molo, Kimani Kuria ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya Bunge la Kitaifa, Wakenya waliokuwa wakithibitisha nambari yake ya simu walimtumia Sh168,000.

Mnamo Jumatano, afisi ya Kamishna wa Kulinda Data iliwaonya Wakenya dhidi ya kusambaza hadharani taarifa za kibinafsi za watu wengine.

Alisisitiza kwamba baadhi ya habari zilizosambazwa ni pamoja na majina, nambari za simu, mahali, na maelezo ya watu wa familia.

Lakini Wakenya walipuuza na hata kusambaza nambari za simu za kamishna wa data.