Habari za Kitaifa

Wacheni ghasia, tuko sawa Kenya, asema Rais Ruto

Na BENSON MATHEKA June 30th, 2024 2 min read

RAIS William Ruto ametoa wito kwa Wakenya kuepuka ghasia na badala yake kukumbatia mbinu za amani za kushughulikia masuala yanayoathiri nchi.

Rais aliwataka Wakenya kudumisha amani, akisema kuwa ghasia zimesababisha watu kupoteza maisha na uharibifu wa mali.

Alisema Kenya ina nafasi nzuri zaidi ya mabadiliko iwapo wananchi wataungana kukabiliana na changamoto zinazokabili taifa hili.

“Sisi ni watu ambao ni wa taifa moja. Tukikabiliana na changamoto zetu pamoja kwa umoja, tutazitatua, na Kenya itasonga mbele,” alisema.

Alisema hayo wakati wa ibada katika kanisa la Lolgorian Pentecostal Evangelistic Fellowship of Africa (PEFA) katika Kaunti ya Narok.

Wakati huo huo, Rais Ruto alieleza imani kuwa nchi inaelekea katika njia ifaayo, akisema kuwa hatua muhimu zimeafikiwa.

Rais alisema serikali imejitolea kuleta mabadiliko nchini kupitia mipango na sera za kibunifu na za makusudi.

Alisema serikali imepunguza gharama za mbolea, kuongeza uzalishaji na kusababisha kupungua kwa gharama za maisha.

Mfumuko wa bei umeshuka kutoka asilimia 9.8 mwaka 2022 hadi asilimia 4.6 mwezi huu.

Zaidi ya hayo, alisema hatua za serikali zimefanya shilingi ya Kenya kuimarika dhidi ya dola, ambayo kwa sasa inabadilishwa kwa Sh128 kutoka Sh162.

Pia alisema kuwa idadi ya watalii imeongezeka, wakati viwango vya riba vinapungua.

“Nina imani kuwa nchi hii itabadilika kwa sababu tunachukua hatua zinazofaa na tunaenda katika mwelekeo sahihi,” alisema.

Rais Ruto alisema kuna baadhi ya watu ambao hawataki Kenya kustawi, akitolea mfano wale wanaohoji kwa nini Kenya ilikuwa nchi ya Afrika iliyoandaliwa kwa Ziara ya Kiserikali ya Marekani katika kipindi cha miaka 16.

Alisema atafanya maamuzi yanayohitajika ili kuipeleka nchi mbele, huku akieleza kuwa nchi imekwama kwa miongo kadhaa kwa sababu ya viongozi kutofanya maamuzi huko nyuma.

Rais alisema serikali inaanzisha kituo cha teknolojia katika kila wadi ili kupanua fursa kwa vijana katika anga ya kidijitali.

“Lazima tuwe na mpango wa makusudi wa kutengeneza ajira kwa vijana wetu,” alisema.

Aidha, alisema Serikali imepata masoko mapya ya mazao ya kilimo nje ya nchi ili kuongeza mapato ya wakulima.

Rais alisema serikali inaanzisha kituo cha teknolojia katika kila wadi ili kupanua fursa kwa vijana katika kidijitali.

“Lazima tuwe na mpango wa makusudi wa kutengeneza ajira kwa vijana wetu,” alisema.

“Haya ni matunda ya safari zangu mbalimbali nje ya nchi,” alisema.

Rais alipongeza wakulima katika Kaunti ya Narok kwa kuzalisha chakula zaidi ambacho kimeimarisha hali ya utoshelevu wa chakula nchini Kenya

Alisema Serikali inajenga barabara katika kaunti hiyo ili kuhakikisha wakulima wanafikisha mazao yao sokoni kwa urahisi.

Alitangaza kuwa Sh1.8 bilioni zitatumika kuunganisha stima katika Kaunti ya Narok.

Gavana wa Narok Patrick ole Ntutu na aliyekuwa Gavana wa Narok Samuel Tunai walihudhuria ibada hiyo.