Habari za Kitaifa

Waislamu washerehekea Eid-Ul-Adha wito wa umoja na maadili kwa vijana ukitolewa


WAISLAMU nchini walijumuika na wenzao kote ulimwenguni sherehe za Eid-Ul-Adha zinazoashiria kutamatika kwa Hajj huku Kadhi Mkuu Athman Abdulhalim akitoa wito kwa vijana wa Kiislamu kujiepusha na matumizi ya mihadarati.

Kadhi Mkuu aliwataka vijana wayazingatie mafunzo ya dini yanayokataa matumizi ya chochote kinachorejelewa kama dawa ya kulevya.

“Vijana wanapaswa kuzidisha juhudi za kuzingatia imani na mafunzo ya dini ya Kiislamu. Wakome kabisa kutumia dawa za kulevya au kitu chochote kinachorejelewa kama dawa ya kulevya,” Sheikh Abdulhalimu akasema.

Alikuwa akizungumza katika uwanja wa Tononoka jijini Mombasa alikoongoza maombi ya Idd-Ul-Adha. Mwaka huu, zaidi ya mahujaji 1.8 milioni walikongamana jijini Mecca, Saudi Arabia, kushiriki hafla ya siku tano, ya kila mwaka ya Hajj.

Ushauri wake unajiri wakati ambapo mjadala umeshamiri nchini kuhusu matumizi ya miraa na muguka.

Hii ni baada ya kaunti za eneo la Pwani kupiga marufuku au kuweka vikwazo vikali dhidi ya biashara na matumizi ya muguka.

Kaunti hizo ni pamoja na Mombasa, Kilifi na Taita Taveta, zilizopiga marufuku biashara ya zao hilo linalokuzwa kwa wingi katika Kaunti za Embu na Meru.

Nazo Kaunti za Lamu na Kwale zimeweka vikwazo na ushuru mkali kwa wasafirishaji na wauzaji wa muguka.

Hata hivyo, mahakama imeweka kando marufuku hiyo hadi kesi iliyowasilishwa na wakulima wa muguka itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Eid-Ul-Adha (sherehe ya kuchinja) ni mojawapo ya siku kuu kubwa katika kalenda ya Kiislamu pamoja na Eid-Ul-Fitri inayoadhimishwa mara moja kwa mwaka.

Sherehe ya Eid-Ul-Adha huadhimishwa kwa njia ya kuchinja mnyama kama vile mbuzi, kondoo, ng’ombe au ngamia.

Kisha nyama husambazwa miongoni mwa watu wa familia, majirani na watu masikini.

Wakati kama huo, Waislamu huja pamoja kwa maombi katika misikiti yao, hushiriki mlo na wapendwa wao na kutoa misaada ya vyakula kwa wale wenye mahitaji au wasiojiweza katika jamii.

Aidha, sherehe hiyo hutoa kumbukumbu ya hadithi ya Quran ambapo Nabii Abrahamu alijitolea kumtoa kama dhabihu mwanawe Ishmael kuashiria uaminfu wake kwa Mungu.

Wakati uo huo, Kadhi Mkuu Sheikh Abdulhalim pia jana alizungumzia tofauti miongoni mwa Waislamu kuonekana kwa mwezi kwa ajili ya sherehe za Idd-Ul-Adha, huku akisisitiza umuhimu wa udugu.

“Sharti tuungane na kujiepusha na migongano na maneno makali. Uislamu ni dini moja na sharti tusimame pamoja. Huu ni wakati wa sherehe, maombi na kutoa shukrani kwa Mungu. Kwa hivyo, tusiuchanganye na mivutano isiyo na maana na matusi,” akahimiza.

Kauli yake pia iliungwa mkono na Dkt Islam Ahmed Salim, aliyeongoza maombi katika msikiti wa Masjid Ummul Kulthum.

Dkt Salim aliwashauri Waislamu kuwaachia wataalamu suala la kuonekana kwa mwezi huku akihimiza umuhimu wa umoja.