Habari za Kaunti

Wawili wafa kwenye mgodi haramu wakisaka dhahabu kutokana na njaa

Na OSCAR KAKAI July 2nd, 2024 2 min read

HALI ngumu ya maisha ambayo inashuhudiwa nchini imeanza kuhusishwa na vifo vinaripotiwa kufuatia wakazi kusaka dhahabu katika Kaunti ya Pokot Magharibi.

Hii imeweka wazi athari za uchimbaji haramu wa dhahabu na haja ya kuweka mbinu mwafaka za uokoaji wakati wa mikasa kwenye migodi katika eneo hilo.

Haya yanajiri baada ya watu wawili kufariki baada ya kuzikwa wakiwa hai kwenye migodi katika eneo la Kambi Karaya kwenye barabara kuu ya Lodwar – Kitale, Jumatatu.

Tukio hilo la kustaajabisha lilitokea wakati wawili hao walikuwa wakisaka riziki.

Shughuli za kuchuma dhahabu hufanyika kwenye barabara kuu ya Kitale – Lodwar huku wachimba dhahabu wakiweka maisha yao kwenye hatari.

Uchunguzi unaonyesha kuwa shughuli hiyo imevutia hata akina mama na watoto ambao huchimba dhahabu ili kuleta chakula kwa meza kutokana baa la njaa ambalo linaendelea kushuhudiwa katika eneo hilo.

Chifu wa Lokesheni ya Nasolot Michael Mwotor anaseam kuwa wanaume hao wawili walipatwa na mauti baada ya migodi kuwaangukia.

Alisema kuwa migodi hiyo ni hatari akisema kuwa waokoaji waliweza kufikia miili na kwa kuchimba na kufanya shughuli hiyo kuwa ngumu.

Bw Mwotot anasema kuwa baa la njaa limesukuma wakazi kwenye kazi hiyo ambayo ni hatari.

“Wenzetu wanaume walienda kusaka pesa kununua chakula lakini wakafariki,” anasema.

Bw Mwotor aliongeza kusema kuwa waathiriwa walikuwa chini kabisa kwenye migodi.

“Hao huenda kwenye migodi kila siku. Kwa bahati mbaya walifariki. Majirani walisikia kilio chao na kukimba kuwaokoa lakini tayari wawili hao walikuwa wameshakufa,” alisema.

Mkazi wa eneo la Lami Nyeusi, David Domungura anaeleza kuwa wakazi wamegeukia kuchimba dhahabu wapate fedha kutokana na njaa na uhaba wa chakula ambao unashuhudiwa katika eneo hilo.

“Wao husaka dhahabu kila siku na wanauza Sh200 kwa gramu moja. Hali ngumu ya maisha imeathiri kila mtu,” anasema.

Bw Domungura aliitaka serikali kuu kusambaza chakula cha msaada kwa familia ambazo zimeathirika na baa la njaa.

Mbunge wa Sigor Peter Lochakapong ambaye alizuru eneo la mkasa aliwataka wakazi kutafuta mbinu mbadala za kujikimu.

“Tunaomba wakazi wajihusishe kwenye biashara zingine badala ya kuchimba dhahabu,” alisema Bw Lochakapong.

Haya yanajiri baada ya kamati ya kusimamia uchimbaji dhahabu kubuniwa kwenye kaunti hiyo ili kuzuia uchimbaji dhahabu kinyume na sheria ambao umeshamiri katika eneo hilo.

Licha ya onyo kutoka kwa serikali, wanaotafuta riziki kupita kwa kuchimba dhahabu hawajafuata maagizo hayo huku wakiendelea na shughuli hiyo.

Kamishina wa kaunti ya Pokot Magharibi Khaliff Abdullahi anasema kuwa miili hiyo miwili ambayo ilikuwa imekwama kwenye migodi iliondolewa jioni.

Bw Khaliff anasema kuwa kumekuwa na ongezeko la vifo vinavyotokana na uchimbaji migodi na wiki hii serikali itapiga marufuku uchimbaji haramu wa dhahabu kwenye kaunti hiyo.