Habari za Kaunti

Ajabu bunge la kaunti ya Laikipia kuharibiwa ilhali mswada tata ulikuwa Bunge la Taifa

Na JOSIAH MUGO June 30th, 2024 2 min read

SPIKA wa Bunge la Kaunti ya Laikipia anaendelea kukadiria hasara baada ya vijana waliojiita Gen Z kuvamia, kupora na kuharibu mali ya mamilioni ya pesa katika majengo ya afisi hizo.

Huku maandamano na makabiliano yalipokuwa yanafanyika katika Majengo ya Bunge la Taifa Jumanne Nairobi, makabiliano sawa na hayo yalikuwa yanafanyika Laikipia na kusababisha uharibifu mkubwa na ghasia licha ya kuwa kaunti hazikuwa zinahusika na sheria hiyo tata.

Spika Lantano Nabaala alisema vijana wenye hasira waliojitambulisha kama Gen Z walivamia majengo ya bunge na kuyaharibu kwa kurusha mawe.

Bw Nabaala alieleza kuwa waandamanaji hao pia waliharibu magari ya MCAs na ya wafanyakazi kabla ya kuvamia ndani ya chumba cha bunge na kuharibu vitu kadhaa.

Alisema alikuwa ndani ya ofisi yake huko Nanyuki wakati mamia ya vijana walipoivamia ofisi hiyo na kuharibu mfumo wa Hansard uliogharimu Sh60 milioni na mfumo wa CCTV uliogharimu Sh35 milioni. Aliongeza kuwa uharibifu wote unaokadiriwa ni karibu Sh150 milioni.

Alisema vifaa vyote vya umeme viliibiwa na kwamba wamepeleka kikosi cha uchunguzi kufuatilia tukio hilo ili kubainisha hasara kamili iliyopatikana.

Alisema hasara ya zaidi ya Sh150 milioni iliku wakubwa kwa watu wa Laikipia na wawakilishi wao ambao hawakuhusika katika Mswada wa Fedha uliokuwa ukikataliwa.

Wakati huo huo, baadhi ya vijana katika mji wa Nanyuki walitoa malalamiko, wakimshutumu Mbunge wa Laikipia Mashariki, Mwangi Kiunjuri kwa kuwatishia kwa madai ya kuongoza maandamano ambayo yalisababisha uharibifu mkubwa wa majengo.

Patrick Wahome alidai kuwa mbunge alimpigia simu na kumtishia kwa kushiriki katika maandamano dhidi ya Mswada wa Fedha.

Wahome, aliyesindikizwa na viongozi wengine wa vijana, alisema amepeleka malalamiko yake katika kituo cha polisi cha Nanyuki.

Vijana hao walidai walikuwa wakipokea vitisho mara kwa mara kwa kukataa Mswada ambao ulikuwa ukisukumwa na utawala wa Rais William Ruto.

Aliongeza kuwa ni jambo lisilokubalika kwa kiongozi anayeheshimika kuwatishia kwa kutoa maoni yao kuhusu Mswada wa Fedha.

Alitaka Serikali iwahakikishie ulinzi badala ya kuwatishia wao na familia zao.