• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 4:28 PM
‘MCAs hufyonza fedha za umma bila kufanya kazi’

‘MCAs hufyonza fedha za umma bila kufanya kazi’

Na ANITA CHEPKOECH

YAMKINI idadi kubwa ya madiwani nchini hugharimu mlipaushuru kiasi kikubwa cha pesa ilhali utendakazi wao ni duni mno.

Msimamizi wa Bajeti (CoB) Agnes Odhiambo alipendkeza idadi ya madiwani ipunguzwe akisema, madiwani hao 2,225 huchangia ongezeko la mzigo wa mishahara ya watumishi wa umma.

Alidai wengi wao hawafahamu vyema jukumu lao kuu la kukagua na kutathmini bajeti na matumizi ya fedha za umma katika kaunti wanazosimamia.

Bi Odhiambo aliiambia Jopokazi la Mpango wa Maridhiano (BBI) lililobuniwa na Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga kwamba, katiba inapasa kufanyiwa marekebisho ili kupunguza idadi ya madiwani kusudi mzigo wa ulipaji mishahara upungue.

“Mabunge ya kaunti ni taasisi zilizopewa majukumu makubwa. Yanapaswa kuchanganua bajeti za kaunti, kuyafanyia marekebisho na kuyaidhinisha. Lakini inashangaza kuwa bajeti hizo hupitishwa katika kikao kimoja tu,” akasema Bi Odhiambo.

“Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti hufanya kikao, huchunguza bajeti iliyopendekezwa kwa saa moja na kisha kuwasilisha katika kamati ya bunge lote ambapo hupitisha baada ya kujadiliwa kwa kikao kimoja,” akaeleza alipotoa maelezo kuhusu namna ya kuimarisha asasi za kufanikisha ugatuzi katika hoteli ya Intercontinental, Nairobi.

Bi Odhiambo alisema licha ya kwa kwamba utendakazi wa asasi za utawala ni sehemu muhimu ya ugatuzi, utendakazi wa asasi hizo hizo kama vile mabunge ya kaunti ni ya kutiliwa shaka kwani hayaridhishi.

Msimamizi huyo wa bajeti aliwaambia wanachama wa jopokazi hilo, wakiongozwa na naibu mwenyekiti Adams Oloo kwamba, angehimiza idadi ya madiwani ipunguzwe, akisema wao ni mzigo kwa uchumi wa nchi.

“Ugatuzi utafanyakazi vizuri ikiwa idadi ya wawakilishi hawa itapunguzwa ili pesa nyingi zielekezwe kwa miradi ya maendeleo,” Bi Odhiambo akasema.

Kujiongeza mshahara

Wakati huo huo, Bi Odhiambo aliwakashifu wabunge kwa kuendeleza mtindo wa kujiongezea mishahara na marupurupu kila mara licha ya kupanga kwa mzigo wa ulipaji mishahara.

“Majuzi tulisoma kwamba wabunge wamejiongezea marupurupu ya nyumba ilhali mishahara yao tayari iko juu. Hatua kama hii haikufaa kwa sababu ni mzigo mkubwa kwa walipa ushuru,” akasema.

Bi Odhiambo pia alipendekeza kuimarisha kwa ushirikishi wa umma katika masuala ya utawala akisema shughuli hiyo haijakuwa ikiendeshwa inavyohitaji kikatiba.

“Kwa mfano, kuna ushirikishi finyu wa wananchi katika mchakato wa utayarishaji wa bajeti za kaunti. Maafisa husika wanafaa kutambua kuwa michango ya wananchi inapasa kushirikishwa wakati wa kuendesha zoezi hilo,” akasema.

Akijibu maswali kutoka kwa wanachama wa jopo hilo, Bi Odhiambo alitetea afisi yake dhidi ya madai kuwa imekuwa ikichelewa kuwasilisha fedha kwa serikali za kaunti, akisema Hazina Kuu ndio inapasa kulaumiwa kwa hitilafu hiyo.

“Pesa hucheleweshwa na Hazina ya Kitaifa. Ni wajibu wao kutafuta pesa na kuziweka katika Hazina ya Serikali za Kaunti. Kazi yetu ni kuidhinisha matumizi ya pesa hizo, kazi ambayo sisi hufanya baada ya kupokea ombi kutoka kaunti husika na kuhakikisha stakabadhi hitajika ni sawa,” akasema Bi Odhiambo.

You can share this post!

Wanachama wa Urithi Housing Co-operative wahimizwa kuchukua...

Waziri akiri serikali ilitoa hati kimakosa

adminleo