Bambika

Gachagua amtania Rais Ruto kwa ‘Uzungu’ wa kumshika mkono Mama wa Taifa

May 30th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

NAIBU Rais Rigathi Gachagua mnamo Alhamisi amemshukuru Rais William Ruto kwa kuwafafanulia wanaume wa Kenya kwamba mtindo wa kushikana mikono hadharani na wake zao ni wa Kizungu wala sio wa Kiafrika.

Akihutubu katika hafla ya maombi ya kitaifa ya kila mwaka ambayo huandaliwa na Bunge la Kitaifa, Bw Gachagua alichukua nafasi yake ya kumwalika Rais kuhutubu kumtania mdosi wake kutokana na ziara yake rasmi nchini Amerika iliyochukua siku nne kati ya Mei 20 na Mei 24, 2024.

Bw Gachagua alisema kwamba Wakenya walikuwa wakifuatilia kwa makini ziara ya kiongozi wan chi na iliyokuwa ya kufana sana.

“Ulitushindia manufaa kemkem lakini kuna shida ambayo ilitokea hapa nchini kutokana na ziara hiyo hasa pale tulikuona ukitembea hadharani ukiwa umeshika mkono wa Mama wa Taifa Rachel Ruto,” akasema Bw Gachagua.

Bw Gachagua alisema kwamba hali hiyo ya kumshika Mama Rachel mkono hadharani ilizua msukosuko katika familia nyingi nchini huku mabibi wetu pia nao wakidai tuwaonyeshe mapenzi sawa na hayo.

“Shida hiyo ilipenya hadi kwangu nyumbani ambapo mke wangu, Pasta Dorcas Rigathi, alianza kudai niwe nikimshika mkono akitoka nyumbani hadi kwa gari lake na hata katika boma letu niwe nikifanya hivyo mara kwa mara,” akasema Bw Gachagua.

Naibu Rais aliongeza kwamba shida sawa na hiyo ilikuwa imejipenyeza kwa Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi ambaye “alinidokezea kwamba pia kwake kulikuwa kumezuka suala la mkewe kumtake aige mfano wa Rais wa kumshika mkono hadharani”.

Alisema kwamba “kwa kawaida mimi na Bw Mudavadi hutambuana kwa jina la Omwami (jina la Kibanyore ambalo humaanisha mwanamume wa hadhi) na aliniuliza kama kwangu hali hiyo ilikuwa imeniletea shida na ndipo nikamuelezea kwamba kwangu ndiko kulikuwa kumegeuka kuwa makao makuu ya hilo”.

Soma Pia: Nilitumia Sh10m pekee kwa ziara ya Amerika – Ruto

Bw Gachagua aliendelea kusema kwamba hakuingiwa na wasiwasi kuhusu hali hiyo kwa kuwa “nilijua kwa uhakika na bila taswishi kwamba Rais ukisharejea hapa nchini ungetutatulia shida hiyo ambayo ulikuwa umetuletea na sikuwa nimenoa kwa kuwa leo hii umetupa mwelekeo wa hali halisi”.

“Leo hii wakati tumekupokea hapa katika Mkahawa wa Safari Park na tukikusidikiza hadi ukumbini, ulikuwa ukikanyaga kubwakubwa tukipiga gumzo huku Mama Rachel akiwa nyuma aking’ang’ana kutufikia,” akasema Bw Gachagua.

Bw Gachagua aliongeza kwamba “hali hiyo imetuonyesha kwamba hayo mambo ya kushikana mikono yalikuwa ya kizungu huko ziarani Amerika”.

Naibu huyo wa Rais alimrejelea mkewe Pasta Dorcas, akimhimiza aache presha za kudai kushikwa mkono hapa nchini kwa kuwa Rais ametoa ufafanuzi wa hali halisi kwamba hayo hufanyika tu kule Uzunguni.

“Lakini wewe tulia tu mke wangu kwa kuwa najua hivi karibuni Rais atanituma kwa ziara ya kikazi nchini Amerika na nakuhakikishia kwamba sitakuacha nyuma bali tutaandamana pamoja… na tukiwa huko nakupa thibitisho kwamba nitakushika mkono kila mahali hadharani lakini tukirejea hapa nchini turejelee maisha yetu ya Uafrika yasiyo na hayo madoido,” akasema.

Aidha kiongozi huyo alizidisha utani wake ambapo alimwambia mdosi wake Rais Ruto kwamba “nimepata dokezi kwamba kutokana na hali hiyo ya kushikana mikono hadharani na mke wako, utaitwa katika kikao cha kongamano la wanaume nchini ndio ukaelezee kwa nini ikawa hivyo”.

[email protected]