Makala

Gachagua: Wakenya nisameheni, nimeacha makasiriko

June 3rd, 2024 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

NAIBU wa Rais, Bw Rigathi Gachagua mnamo Jumapili ya Juni 2, 2024 aliwaomba Wakenya msamaha kwa makasiriko ya utengano ambayo alikiri amekuwa nayo, akisema sasa amepona.

“Mimi niliingia kwa ofisi nikiwa mtu aliyekuwa na machungu mengi sana na nilikuwa nimekasirika. Hali hiyo ilikuwa imechangiwa na jinsi nilivyokuwa nimehangaishwa, kudunishwa, kudharauliwa na pia kujeruhiwa moyo wangu na utawala uliokuwepo,” akasema Bw Gachagua.

Aliongeza kwamba maombi ya mkewe kuhusu makasiriko yake ndiyo yamefanya kazi na yakajibiwa na Mungu na akapata uponyaji.

“Nimepona sasa. Namshukuru mke wangu (Pasta Dorcas Rigathi) ambaye ni malkia wa maombi katika maisha yangu. Amekuwa akiniombea kwa muda wa mwaka mzima. Kwa sasa nawatangazieni kwamba nimepona kikamilifu na roho yangu ni safi,” akasema.

Bw Gachagua alisema kwamba kupona huko kwake ndiko kumemshinikiza kuwaomba msamaha wote ambao alikwaruzana nao katika siasa za uchaguzi mkuu wa 2022 ambazo alizitaja kuwa hasi na za kuumizana.

Akiongea katika ibada ya kanisa la Kikatoliki la Timau ndani ya Kaunti ya Meru, Bw Gachagua alisema “sasa mimi nawaomba mnisamehe kwa yale yote ambayo niliwasononesha nayo kwa muda huo, huku nami vilevile nikitangaza kuwasamehe wote walioniweka vidonda hivyo vya machungu”.

Bw Gachagua amekuwa akiomba familia ya mwanzilishi wa Taifa Mzee Jomo Kenyatta msamaha kwa cheche za maneno, dhuluma za kiutawala na pia visa vya magenge kuilenga na kuidhalilisha.

Bw Gachagua alisema kwamba “sasa mimi nimeona mwenge wa amani na utulivu, na ninawaomba Wakenya wote wajumuike kwa mwito wangu wa kuwaomba tusameheane, tukumbatiane na hatimaye tuungane kama nchi moja ili tuafikie ustawi wa kimaeneo na wa nchi”.

Kumemsaidia kufumbua macho

Alisema kwamba kule kupona ambako amepona kumemsaidia kufumbua kwamba watu wanafaa kuishi kama mandugu ndani ya upendo wa dhati.

“Nimeelewa kwamba hata ukimwona dada yako ameolewa na tajiri usimwonee kinyongo bali unafaa ushabikie ndoa hiyo kwa kuwa huenda iwe ndiyo itabeba baraka zako,” akasema.

Wapenzi wa fasihi wametafsiri msemo huo wa Bw Gachagua kumaanisha kwamba hata Rais William Ruto akionekana kuwachumbia kwa dhati wanasiasa kama Raila Odinga, Musalia Mudavadi na Uhuru Kenyatta, yeye kama Naibu wa Rais atakuwa wa kuweka amani pasipo kuingiwa na wasiwasi kwa kuwa huenda umoja huo uishie kumfaa hata yeye mwenyewe.

Bw Gachagua aliyeonekana kubadili mbinu yake ya hotuba ambapo kinyume na kawaida yake ya kupigia debe masilahi ya Mlima Kenya, alisema taifa lote linafaa kuungana ili kuafikia maendeleo.

Alifichua kwamba Rais William Ruto tayari ametoa makataa ya hadi Agosti 2024 kwa Gavana wa Meru Bi Kawira Mwangaza awe ameleta amani kati yake na viongozi wa Kaunti hiyo.

“Mimi nimekuwa nikijihusisha na kutafuta amani ya hapa Meru ambapo kumekuwa na misukosuko tangu 2022,” akasema.
Bi Mwangaza ameng’atuliwa mara mbili na bunge la Kaunti ya Meru lakini bunge la Seneti limemrejesha mamlakani.

“Tulimuita katika mkutano wa masaa matano katika ikulu ambapo Rais alimpa makataa ya miezi mitatu awe amepalilia uwiano kati yake, wabunge na madiwani na kwa sasa niko na uhakika kwamba matunda yameanza kuonekana,” akasema.

Aliwataka wanasiasa wote wa Meru wasameheane ili amani ifungue mianya ya maendeleo ambayo kwa sasa alisema yamekwama.

Bw Gachagua alisema kwamba Mlima Kenya utazidi kuungana na pia uwe huru kufanya mashauriano na maeneo mengine ili kupalilia umoja wa safari ya kisiasa iliyo mbele.