Siasa

Haki ya uwakilishi ndio haki ya mgao wa rasilimali – Peter Kenneth

June 8th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

ALIYEKUWA mwaniaji wa urais mwaka wa 2013 Bw Peter Kenneth, sasa amewataka viongozi kukumbatia mjadala wa kuongeza idadi ya maeneobunge kwa lengo la kusawazisha idadi ya wapigakura kwa kila mojawapo, hii pia ikileta usawa kwa idadi jumla ya watu.

Bw Kenneth ambaye alihudumu kama Waziri Msaidizi katika Wizara ya Mipango ya Kitaifa katika utawala wa Rais Mwai Kibaki (2002-2013) alisema kwamba “maeneobunge ni safu kuu ya ugavi wa rasilimali za kitaifa”.

Akiongea katika eneo la Kirwara mnamo Jumamosi, Bw Kenneth ambaye pia alihudumu kama mbunge wa Gatanga alisema kwa sasa mfumo wa ugavi rasilimali hizo uko na dosari.

“Lakini licha ya kwamba kuna mapendekezo kama suluhu, njia ya kipekee ya kufaulu ni ongezeko la maeneobunge,” akasema Bw Kenneth.

Alisema kwamba “imetambulika kwamba tetesi nyingi zinatokana na migao ya basari na pia vitita vya kufanikisha maendeleo”.

Bw Kenneth alisema kwamba dosari kuu iko katika kuyapa maeneobunge yote pesa zinazotoshana pasipo kuzingatia yale maeneo ambayo yako na watu wengi.

Alisema kwamba eneobunge la Ruiru kwa mfano, lililo na zaidi ya wapigakura 200,000 hupata mgao sawa na eneobunge fulani lililo na wapigakura 10,000.

“Ili kuziba tofauti hiyo, tunafaa kuzingatia mjadala wa kusawazisha idadi ya wapigakura katika kila eneobunge na ndio pesa za maendeleo ziwe na uwakilishi wa wabunge wengi,” akasema.

Alisema ule mjadala ambao umezuka kuhusu ugavi wa rasilimali hizo kwa kuzingatia idadi ya watu hauna ule uwazi kwa kuwa ni kama unalenga kuzua mirengo ya kumenyana kisiasa.

“Mimi sioni uwazi wowote katika mjadala huu. Ni kama kuna wanasiasa ambao wanasaka ajenda ya 2027 na hawana ile nia njema na masilahi ya mwananchi bali wanalenga kuzuke mawimbi ya kuvamiana kiubabe,” akasema.

Bw Kenneth alisema kwamba kwa sasa kumezuka mirengo ya Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, wandani wa Rais William Ruto eneo la Mlima Kenya na pia wakereketwa wa Azimio la Umoja One Kenya Alliance ambao wamehitilafiana hadharani kuhusu mfumo wa kugawa mali.

“Kitu cha kuondoa kabisa katika mjadala huu ni kwamba Mlima Kenya ndio hufinywa na mfumo unaotumika kwa sasa,” akasema.

Alisema kwamba ni kaunti 18 ambazo ziko katika orodha ya kutopata haki ya migao.

“Kaunti hizo ni Nairobi, Kiambu, Nakuru, Kakamega, Bungoma, Meru, Kilifi, Machakos, Kisii, Mombasa, Uasin Gishu, Narok, Kisumu, Migori, Murang’a, Homa Bay, Kitui, na Kajiado,” akasema.

Bw Kenneth alisema kwamba kati ya kaunti hizo, ni tano tu ambazo ziko Mlima Kenya.

“Hizo nyingine zote 13 ziko katika maeneo mengine. Mjadala huu unaweza sasa ukasemwa unalenga kuzua mtafaruku kati ya kaunti 18 dhidi ya 29 hali ambayo haifai kamwe,” akasema Bw Kenneth.

Kiongozi huyo aliongeza kwamba “shida kuu ni kwamba vita vikuu kuhusu mfumo huo vimekita kambi katika eneo la Mlima Kenya na kutuangazia kama wa kujipenda ilhali ni vile tu hawajumuiki katika vikao vya kujadili suala hili kwa uwazi”.

Bw Kenneth alishikilia kwamba kwa sasa ikiwa wale ambao wako wengi lakini bila maeneobunge yaliyo na haki ya uwakilishi wataungana kwanza kupata hiyo haki, basi mjadala huu utakoma kuwa wa farakano.

“Mimi naomba kwanza tuunde Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ndio hatimaye tupate makamishna wa kuandaa harakati za kutathmini upya mipaka nchini na hapo ndipo kaunti hizo 18 zinafaa kuwasilisha lalama zao,” akasema.