Habari Mseto

Hamasisho wanafunzi wa kike wawe marubani

June 17th, 2024 2 min read

Na FRIDAH OKACHI

WANAWAKE katika sekta ya usafiri wa ndege wapo mbioni kuhakikisha idadi yao inaongezeka kwa kutoa mafunzo kwa taasisi mbalimbali za masomo nchini.

Wakilenga shule za upili na hasa wanafunzi wa kike walio katika kidato cha kwanza na pili, wanatoa hamasisho hilo kupitia Shirika la Girls in aviation Africa (GIAA).

GIAA ni muungano wa marubani na wahandisi kwenye usafiri wa ndege nchini ambao hutoa ushauri na mafunzo kwa wanafunzi.

Wakati wa kutoa ushauri kwa wanafunzi wa Shule ya Wasichana ya Ngara, mjini Nairobi, wikendi, Mkurugenzi wa GIAA, Bi Juliet Mutua alisikitika kwamba wanawake wengi wamenyimwa fursa ya kazi za urubani kwa sababu ya kuchukua likizo ya kujifungua na kulea watoto, kinyume na wanavyochukuliwa wanaume.

Akisimulia wakati mgumu wa kupata nafasi kwenye sekta hiyo ya usafiri, alisema alipitia dharau kutoka kwa kampuni moja hadi nyingine.

“Wengi hawataki kuajiri mwanamke kwa sababu atapata ujauzito halafu asalie nyumbani kwa kipindi cha miaka miwili ndiposa arejee kazini. Binafsi niliambiwa nafasi niliyotafuta itamfaa mwanamume ambaye hana wakati wa kulea watoto,” alisema Bi Mutua.

Bi Mutua, ambaye ni mhandisi mwenye tajriba ya miaka 15, alikosa kukata tamaa na hivyo anafurahia safari hiyo yenye manufaa baada ya changamoto nyingi.

“Kama mwanamke ilibidi nifanye kazi mara mbili zaidi ya mwanaume ili kuonyesha mabosi ninafaa,” alidokeza

Bi Mutua alihimiza kuboreshwa kwa sera, akiwataka waajiri kuwapa wanawake nafasi hizo.

“Ni changamoto kubwa, kati ya wanaume 100 tunataka wanawake 10 waajiriwe. Wakati umefika tuweze kuketi kwenye majopo, tupewe nafasi ya kutoa mafunzo kwa shule za marubani.”

Utafiti uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) unaonyesha kuwa duniani ni asilimia 4 ya wanawake wanaotoa huduma za urubani na asilimia 5 hutoa huduma za kudhibiti trafiki, uhandisi na matengenezo.

Mwanzilishi wa GIAA Bi Maseka Semo-Olesi Kithinji ambaye pia ni rubani, alisema vuguvugu hilo la wanawake linalenga wanafunzi wa kidato cha kwanza na pili ili kuwavutia wakati wa kufanya maamuzi ya kazi za baadaye.

Rubani huyo ambaye pia ni wakili alisema kufikia sasa wametoa ushauri kwa wanafunzi 6,000 katika kaunti tano.

“Taaluma hii ni ghali sana. Leseni pekee ni gharama kubwa. Tunapotoa mafunzo haya,  tunatazamia kushirikiana na serikali kupitia Kikosi cha Wanajeshi Angani (Kenya Airforce) na Ulinzi ili wakimaliza shule inakuwa ni chaguo lao,” aliongeza Bi Maseka.

Mpango huo unaoleta pamoja mashirika tofauti, unahusisha mtaala pana unaowatambua wanafunzi kwa misingi ya usafiri  na uhandisi wa anga.

Mkuu wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Ngara Bi Beatrice Ndiga Odiero, alisema lengo lao ni kuvunja vizuizi na dhana potovu ambazo zimepunguza ushirika wa wanawake katika urubani.

“Hili ndilo eneo ambalo halijazingatiwa zaidi. Tumekuwa tukileta wahadhiri kutoka vyuo tofauti kujadili taaluma zingine,” alisema Bi Odiero.

Mpango huo tayari unazua msisimko miongoni mwa wanafunzi.

Mary Njoroge, mwanafunzi wa kidato cha pili, alielezea imani yake kuwa ipo siku ataafikia ndoto zake. “Natamani kuwa rubani lakini sikuwahi kufikiria kuwa inawezekana kwa mtu kama mimi. Ushauri huu umenipa ujasiri na maarifa ya kutekeleza ndoto yangu.”