Siasa

Hofu ya Rais Ruto kuhusu uchaguzi wa UDA Nairobi

June 5th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

RAIS William Ruto sasa ameamrisha kuahirishwa kwa uchaguzi wa mwenyekiti wa chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) katika Kaunti ya Nairobi, ikiaminika kwamba hatua hiyo inalenga kuzima mpasuko ambao unanukia katika vita vya ubabe kati ya mrengo wake na ule wa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Haya yamefichuliwa na mwandani wa Bw Gachagua ambaye ni mbunge wa Embakasi Kaskazini Bw James Gakuya, na ambaye anawania wadhifa wa uenyekiti dhidi ya Gavana Johnson Sakaja.

Aidha, Katibu Mkuu wa muda Bw Cleophas Malala amethibitisha kwamba uchaguzi huo wa mwemyekiti wa UDA Nairobi ulikuwa ufanyike Ijumaa ijayo “lakini kwa kuzingatia mikakati ya kuimarisha demokrasia na umoja miongoni mwa wadau, ikaamuliwa kwanza tuahirishe shughuli hiyo”.

Baada ya uchaguzi wa mashinani wa Kaunti ya Nairobi ambapo wadi na maeneobunge yalichagua wenyeviti wao, orodha ya wajumbe 340 walionasa viti vya mashinani Nairobi walikuwa wakongamane na wamchague mwenyekiti wao ambapo Bw Gachagua anawakilishwa na Bw Gakuya huku nao mrengo wa Dkt Ruto ukiwa na bendera kupitia Bw Sakaja.

Bw Sakaja na Bw Gakuya wamekuwa wakitoa taarifa za kutatanisha kuhusu ubabe wao ndani ya orodha hiyo ya wajumbe.

Huku Bw Sakaja akidai kwamba orodha hiyo iko na wandani wake 240, Bw Gakuya anashikilia kwamba yeye ndiye kichwa kwa kuwa na 248.

“Rais alituambia tusichaguane kwanza hadi wakati ule ambapo atarejea kutoka ziara yake rasmi katika taifa la Korea Kusini. Lengo ni kwamba anataka akutane na wawaniaji wa wadhifa huo na kuwe na mazungumzo ya kuimarisha chama. Ametuagiza kwanza tusikikimbie kuandaa uchaguzi huo katika mazingira yaliyoko kwa sasa na tumetii. Lakini tuko macho kwa kuwa hatutakubali hadaa zozote na njia zozote za mkato za kutunyima haki ya kidemokrasia,” akasema Bw Gakuya.

Bw Malala alisema hakuna mpasuko ulioko katika chama cha UDA, bali “ni demokrasia inajidhihirisha na mambo yatakuwa sawa katika siku za usoni”.

Bw Sakaja alisema shughuli ya kumchagua mwenyekiti wa Nairobi inalenga kukipa chama cha UDA uthabiti wa kuunganisha jamii zote za kaunti hiyo wala sio kuridhisha wengine huku nao wengine wakibaguliwa au kutengwa.

“Ni wakati wa kuunganisha wakazi wote wa jiji la Nairobi pasipo kuzingatia mirengo ya kijamii na vyama. Nairobi ni nyumbani kwa kila mtu na hakuna vile tunaweza tukakubali kushinikizwa tuwe wa kufuata maneno ya kudunisha na kudharau wengine na kuwageuza kuwa wageni katika taifa lao,” akasema Bw Sakaja.

Mvutano kati ya mirengo ya Rais Ruto na Bw Gachagua imeingiwa hata na upenyo wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya ambao ndio huwa na usemi mkuu katika Kaunti ya Nairobi.

Bw Sakaja tayari amekiri kwamba hawezi akatekeleza majukumu yake kama Gavana bila kunyenyekea ushirikiano wa Azimio “kwa kuwa hata katika bunge langu wao ndio wengi… hivyo basi kufanya siasa zetu kuwa na mseto wa mirengo yote, kinyume na hali nyingine ambapo kunao wanatutaka tufikirie kama watu wa jamii fulani”.

Bw Gakuya tayari amedokeza kwamba “iwapo Rais Ruto atapendekeza kuwe na uwiano ambao utakaidi demokrasia ya kuchaguliwa kwa wajumbe 340 na ambao ndio wanafaa kuachiwa jukumu la kumchagua mwenyekiti wao, basi aelewe tutamwonyesha kisogo Nairobi na hali hiyo tuitandaze hadi maeneo ya mashinani Mlima Kenya”.

Ikiwa vitisho hivyo vitaishia kutekelezwa, wadadisi wa masuala ya kisiasa wanaamini kwamba Rais Ruto na Bw Gachagua hawatakuwa pamoja katika uchaguzi wa 2027 na Mlima Kenya huenda uwe katika muungano mwingine.