Siasa

Hotuba ya Rais: Wengi walitarajia atoe nyaunyo kwa makateli serikalini

May 3rd, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

BAADA ya serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto kukabiliwa na changamoto tele katika siku za hivi karibuni, alipotangaza kwamba angehutubia taifa mnamo Ijumaa, matumaini yalikuwa kwamba angetangaza msimamo wa kutikisa.

Masuala nyeti ambayo yanasumbua serikali kwa sasa ni mafuriko ya mauti, mgomo wa wauguzi, ajali za barabarani, maongezi ya ovyo kutoka kwa baadhi ya washirika wake, kashfa za ufisadi ikiwemo ile ya mbolea ya ruzuku na pia ugaidi.

Mawaziri kadha wa serikali yake wamekuwa katika kichinjio cha kudadisiwa kuwa wazembe, wafisadi na wa kufanya ubaguzi na mapendeleo katika ajira huku wengine kama Waziri wa Kilimo Bw Mithika Linturi akiwa katika hatari ya kushtakiwa na kung’atuliwa.

Waziri wa Kawi Bw Davis Chirchir amekuwa wa kushuhudia Wakenya wakitumbukia gizani baada ya stima kupotea kiholela.

“Kuna changamoto nyingi nchini na nilitarajia mjeledi wa Dkt Ruto wa kuwafuta kazi wasiomfaa katika kuzingatia vigezo vya utawala bora. Nilikuwa ninatarajia Dkt Ruto ajitokeze kwa ukali akitangaza kuwa yametosha Wakenya kuchukuliwa kimzaha. Lakini wapi!” akasema Bw Jeremiah Kioni, ambaye ni aliyekuwa mbunge wa Ndaragwa.

Bw Kioni alisema kwamba “kile nimesikia cha kusikitisha zaidi ni kiongozi fulani kudai kwamba “haya mafuriko ni maombi ya wakulima yaliyotimizwa”.

Aidha, Bw Kioni alisema kwamba alitarajia kumsikia kiongozi wa nchi akitangaza ni hatua gani ambazo angewachukulia mawaziri na makatibu wazembe, wafisadi, wa kutoa ajira bila kuhusisha taasisi zinazohitajika na pia wale ambao wamekuwa na lugha ya dharau na majivuno kwa wananchi.

“Yale Rais aliyotangaza ni yale mambo ambayo yangesemwa na mawaziri wake hasa yule wa Elimu Bw Ezekiel Machogu ambaye hata huwa anatoa taarifa rasmi mwendo wa saa saba usiku. Huyo ndiye ambaye angetumwa kutangaza kwamba shule zitabakia kwa likizo hadi serikali itangaze tarehe mpya ya kufunguliwa,” akasema aliyekuwa Waziri Msaidizi wa Elimu na Spoti Bw Zack Kinuthia.

Bw Kinuthia alikejeli kwamba “wakati Wakenya wanalia ndani ya mafuriko, wengine wanakimbia kwa wahasiriwa wa janga hilo ili kumenyana kisiasa”.

Alikuwa akirejelea hali ya Aprili 30, 2024, ambapo Naibu Rais Rigathi Gachagua na mbunge wa Kiharu Bw Ndindi Nyoro walionekana wazi kubishania haki za kisiasa kuhusu wahanga saba waliokufa katika janga la maporomoko ya ardhi ndani ya kiijiji cha Kiganjo, eneobunge la Mathioya.

Aliyekuwa mbunge wa Gatanga Bw Nduati Ngugi alisema kazi ya kuongoza nchi ni ngumu na matarajio ya Wakenya kwa sasa yako katika ile hali ya taharuki na hasira.

“Katika mazingara ya uchumi kuwa mgumu na ambapo ajira na biashara zinapotea, huwezi ukaja kwa Wakenya ukiongea kuhusu yale masuala ya kawaida ambayo wanajua yako. Wanatarajia kumwona rais wao akijitosa katika changamoto hizo akizomea na kuadhibu waliozembea,” asema.

Bw Ngugi alisema kwamba “tunajua waziwazi kwamba shida ya mafuriko imekumba wanyonge wengi ambao kwa msukumo wa umasikini au kufathiliwa na wanasiasa, wamejenga katika kingo za mito na pia kando mwa mabwawa”.

Bw Ngugi alisema “ni hali ya kusikitisha kuwasikia mawaziri wa serikali wakiongozwa na Rais na naibu wake wakitoa onyo kwamba watu hao wajiondoe kwa hiari hadi maeneo salama la sivyo wafurushwe kwa mabavu”.

Bw Ngugi alisema kwamba “utu na utawala bora ni kuelewa kwamba hao watu hawana kwa kwenda na ni jukumu la serikali kuwaonyesha watakapokwenda kukita kambi na mazingara ya wanakohamishiwa yawe ya kuzingatia vigezo vya haki za kibinadamu”.

Hata hivyo, walio katika utawala wa Rais Ruto wakiongozwa na kinara wa wengi bungeni Bw Kimani Ichung’wa walisema kwamba hotuba ya rais ilitoa mwongozo wa busara kwa masuala nyeti.

Bw Ichung’wa alisema kwamba “hotuba ya Rais ilikuwa na busara kama ya Mfalme Suleiman wa Biblia hasa katika kujali masilahi ya wanafunzi”.

Hayo yakiendelea, Rais hakuzingatia hata kero ya ugaidi ambapo mnamo Jumatano, kikosi cha usalama katika msitu wa Boni, kwa mujibu wa ripoti maalum ya kitengo cha kupambana na ugaidi (ATPU), “watu sita akiwemo Mzungu walipigwa risasi na kuuawa wakiwa katika njama ya uvamizi wa kigaidi nchini”.

Ni katika hali hizo ambapo wengi, hata raia kwa mitandao ya kijamii wanamdhania Rais wao kutowajibika katika kutoa matangazo ambayo yanaridhiana na hali halisi inayochochea matarajio ya Wakenya.

[email protected]