Habari za Kitaifa

Jeshi lilivyoshika doria bila kudhuru umma, kinyume na walivyohofia wengi

Na BENSON MATHEKA June 28th, 2024 2 min read

MAAFISA wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) jana Alhamisi walionyesha uungwana wa kikazi walipotumwa kushika doria katika jiji la Nairobi kusaidia polisi kukabiliana na waandamanaji.

Wanajeshi walipelekwa kufuatia hatua ya Bunge kuidhinisha kutumwa kwao kusaidia kuzima waandamanaji waliovamia majengo ya Bunge mnamo Jumanne.

Rais William Ruto alitaja kitendo hicho kama uhaini na kuapa kutumia nguvu zote za serikali kukabiliana na wahusika.

Waziri wa Ulinzi Aden Duale alichapisha ilani katika gazeti rasmi la serikali kutangaza kutumwa kwa wanajeshi kusaidia polisi na kulinda majengo na ofisi za serikali.

SOMA PIA: Wacha jeshi lisaidie polisi kupambana na waandamanaji, mahakama yaamua

Ilitarajiwa kuwa wanajeshi hao ambao huogopewa sana kwa kutumia nguvu hawangewahurumia waandamanaji.

Jana, magari ya kijeshi yalikuwa yakishika doria katika majengo ya Bunge na barabara zilizochaguliwa zikiwemo za kuelekea Ikulu ya Nairobi ambako waandamanaji walitarajiwa kuelekea.

Tofauti na polisi waliokabili vijana waliokuwa wakiandamana kwa amani na bila silaha kwa kuwarushia vitoa machozi kuwatawanya, wanajeshi hawakubanduka katika magari waliyotumia kupiga doria jijini.

Waandamanaji waliwapongeza maafisa wa KDF

Baadhi ya waandamanaji waliwapongeza maafisa wa KDF wakisema waliwatumia kujikinga dhidi ya ukatili wa maafisa wa polisi ambao wamelaumiwa kwa kuendelea kutumia nguvu kupita kiasi.

Uungwana wao ulishuhudiwa walipoingia katikati ya jiji kutoka barabara ya University Way na kupitia katikati ya waandamanaji waliozingira gari lao wakiimba nyimbo za kushinikiza serikali ya Rais William Ruto ijiuzulu.

Huku wakionyesha utulivu wa kitaaluma, wanajeshi hao waliokuwa wamejihami hawakushuka katika gari lao na kuwaacha waandamanaji wakiendelea kueleza hasira zao dhidi ya serikali.

Hata hivyo, baada ya kuondoka, milipuko kadhaa ilisikika polisi wakiwarushia vitoa machozi vijana hao ambao hawakuwa na silaha. Milio ya risasi pia ilisikika polisi walipokuwa wakiwakabili waandamanaji.

SOMA PIA: Uhalali wa amri ya kutuma jeshi kukabili maandamano watiliwa shaka

Katika uwanja wa michezo wa Nyayo ambako wanajeshi hao walikuwa wakisubiri amri iwapo huduma zao zingehitajika kusaidia wenzao waliokuwa katikati ya jiji, shughuli katika barabara za karibu za Uhuru Highway na Lang’ata ziliendelea kama kawaida.

Licha ya kutumwa kukabiliana na raia wakiandamana, maafisa wa kijeshi sawa na polisi wanapaswa kuzingatia haki za binadamu za Wakenya wakiitwa kusaidia machafuko ya raia.

Kutumwa kwa KDF kulitangazwa kwenye gazeti la serikali Jumanne, Juni 25 na Waziri wa Ulinzi Aden Duale kufuatia maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha ambayo yalizua taharuki, hadi Bungeni.

Hata hivyo, hatua hiyo imepingwa na Chama cha Wanasheria nchini (LSK) na makundi mengine ya kiraia ambayo yanasema kuwa kutumwa huko ni kinyume cha katiba.

SOMA PIA: Bunge la ‘waheshimiwa’ lilivyokosewa heshima na kufanyiwa uharibifu ulioacha wengi vinywa wazi

Jana, shughuli zilikwama katika jiji la Nairobi waandamanaji walipokabiliana na polisi. Licha ya Rais kukataa kutia saini Mswada wa Fedha wa 2024 ambao vijana walipinga, jana walimiminika katika miji kadhaa nchini kuelezea hasira zao na utendakazi wa serikali na wabunge.

Maandamano yalifanya katika miji ya Mombasa, Kisumu, Kisii, Homa Bay, Makueni, Kilifi, Kakamega lakini idadi kubwa ya maafisa wa kijeshi walitumwa Nairobi.

Licha ya maafisa hao kukabiliana na waandamanaji katika mchezo wa panya na paka katikati ya jiji kwa zaidi ya saa saba, wanajeshi hawakuingilia kati.

Waandamanaji kadhaa walikamatwa na polisi wakiwemo waliovalia kiraia.