Makala

Juhudi za Azimio kudandia uasi wa Gen Z

Na BENSON MATHEKA June 23rd, 2024 2 min read

WANASIASA wa upinzani wanajitahidi kudandia maandamano ya vijana wa kizazi kipya maarufu Gen Z ambao wanapinga Mswada wa Fedha 2024 ulio na mapendekezo ya ushuru utakaowaumiza huku juhudi za viongozi hao zikionekana kugonga mwamba.

Kwa wiki moja sasa, vijana hao wamekuwa wakipanga na kushiriki maandamano ya amani wakijitokeza kwa maelfu huku wakiwataka vigogo wa upinzani chini ya uongozi wa aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga waliozoea kuitisha uasi wakae kando.

“Raila usiseme kitu, ulitekeleza jukumu lako, tuachie uwanja sasa,. Tunakataaa Mswada wa Fedha 2024,” mmoja wa waandalizi wa maandamano ya Jumanne jijini Nairobi alimwambia Raila kupitia mtandao wa kijamii ambao wamekuwa wakitumia kupanga uasi dhidi ya serikali.

Raila aliyekuwa nje ya nchi alionekana kufurahishwa na juhudi za vijana. “ Leo, mimi najivunia kuwa baba,” alisema akipongeza msichana aliyemtaka asidandie maandamano yao ambayo yalianza Nairobi kabla ya kuenea katika miji zaidi ya 21 kote nchini kufikia Ijumaa.

Hata hivyo, vinara wenza wa Raila katika upinzani wakiongozwa na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Martha Karua wa Narc Kenya, Eugene Wamalwa wa DAP Kenya na katibu mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni wamekuwa wakijaribu kudandia maandamano hayo.

Viongozi hao ambao kwa muda walikuwa wakitishia kurudi barabara kuandamana bila vitendo tangu Raila alipoingia baridi baada ya kutangaza azma yake ya uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika inayoungwa mkono na serikali, wamekuwa wakihimiza vijana hao kuandamana.

Mnamo Alhamisi, Bw Kioni aliashiria kuwa Jubilee ingejiunga na maandamano ya vijana hao lakini wakamwambia acheze mbali.

Wakiwapongeza vijana kwa kuandamana kushinikiza serikali, viongozi wa upinzani wamekuwa wakiwahimiza kubandua wabunge wanaounga mswada huo huku wakikashifu maafisa wa polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji. Mnamo Ijumaa, vijana katika baadhi ya maeneo waliandamana hadi afisi za wabunge wao maeneo yao waliounga mswada huo kuonyesha hasira zao.

Naye Bw Musyoka aliongoza vinara wenza wa Azimio kukashifu polisi kwa kutumia nguvu kupitia kiasi dhidi ya vijana wanaoandaa na kushiriki maandamano ya amani. Kufikia Ijumaa, vijana wawili waliripotiwa kufariki kufuatia majeraha waliyopata kwa kupigwa na maafisa wa polisi Alhamisi jijini Nairobi.

“Kama Azimio na kwa niaba ya watu, tunataka Inspekta Jenerali wa Polisi Japheth Koome na Kamanda wa polisi Nairobi Bw Adamson Bungei wajiuzulu mara moja kwa kushindwa kulinda vijana waliokuwa wakiandamana kwa amani. Tunataka Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kuwafungulia mashtaka Koome, Bungei, na maafisa wenzao katili waliomuua Rex (Masai),” alisema Bw Musyoka, wakati Azimio iliandaa kikao cha wanahabari jijini Nairobi Ijumaa. Rex ni mmoja wa vijana wawili waliofariki kutokana majeraha ya kupigwa na polisi wakiandamana.

Mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki anasema Azimio inatafuta kila mbinu kudandia maandamano yanayoonekana kufaulu ya vijana japo anahisi kuwa kuna mkono wa wanasiasa katika uasi huo.

“Kwa kuwa maandamano yanafaulu kuvutia maelfu ya vijana kote nchini, wanasiasa wa upinzani wakajaribu juu chini kujijhusisha nao na kuyatumia kuendeleza maslahi na azima zao kuelekea 2027 lakini vijana wanaonekana kuwapa ujumbe tofauti kwamba wanataka kuchukua mwelekeo wao wenyewe. Kwamba huu ni wakati wetu na tunaweza kupigania haki zetu na kwamba tunajua mbinu ya kufanya hivyo,” asema Gichuki.

Anasema kwamba sio ajabu kuna usaidizi wa vigogo wa kisiasa wa chini ya maji kufanikisha maandamano hayo.

“Wanachohofia wanasiasa hawa ni kuwa huenda wimbi la sasa la mwamko mpya wa vijana likawaondoa katika siasa za nchi hii. Hii ndio sababu wanajaribu kudandia maandamano hayo hima kwa kuyafadhili chini ya maji au kwa kutoa kauli za kuwahimiza na kulaani ukatili wa polisi dhidi yao,” alisema Gichuki.