Siasa

Mejja Donk: Nitamuunga mkono Babu Owino kwa ugavana Nairobi

May 18th, 2024 1 min read

NA CHARLES WASONGA

AZMA ya Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino ya kutwaa wadhifa wa Ugavana wa Nairobi mwaka 2027 imepigwa jeki kwa kupata uungwaji mkono kutoka kwa Mbunge wa Embakasi ya Kati Benjamin Gathiru almaarufu Mejja Donk.

Kwenye kanda ya video inayosambaa mitandaoni, mbunge huyo aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Rais William Ruto, anasema atamuunga mkono Bw Owino ikiwa ataidhinishwa na Azimio La Umoja-One Kenya kuwania kiti hicho katika uchaguzi huo.

“Saa nyingine tukiwa na Babu huwa ninamuita Gavana… Ninatangaza hapa kuwa ikiwa kinyang’anyiro kitakuwa kati ya Babu katika Azimio na Sakaja (Gavana Johnson Sakaja) katika Kenya Kwanza, nitamfanyia kampeni Babu,” akasema Bw Gathiru.

Mbunge huyo ni miongoni mwa wabunge wa UDA kutoka Kaunti ya Nairobi ambao wanamsuta gavana Sakaja kwa utendakazi mbaya tangu alipoingia ofisini mwaka 2022.

Wengine ni John Kiarie (Dagoretti Kaskazini), James Gakuya (Embakasi Kaskazini) na Augustine Kamande (Roysambu).

Kwenye kanda hiyo ambapo anaonekana akihutubia mkutano fulani wa hadhara katika eneobunge la Embakasi Masharaki, mbunge huyo anasema chanzo cha asilimia 90 ya matatizo yanayowazonga wakazi wa Nairobi yanatokana na utepetevu katika utendakazi wa serikali ya Gavana Sakaja.

“Hizi shida mnazolalamikia zinafaa kusuluhishwa na serikali ya kaunti. Kabla ya hapa tumekuwa Dagoretti na shida ni hizo hizo za taka kutapakaa kila mahali, usambazaji wa maji kwa vipimo, ukosefu wa dawa katika hospitali za kaunti miongoni mwa nyingine,” akasema.