Habari za Kitaifa

Mtego wanasa wasiokuwapo: Kitoa machozi kilivyolipukia Coast Girls na kujeruhi wanafunzi 15


KARIBU wanafunzi 15 katika Shule ya Upili ya Coast Girls mjini Mombasa walijeruhiwa baada ya kitoa machozi kulipuka karibu na shule hiyo wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha wa 2024/2025.

Kisa hicho kilitokea wakati maafisa wa polisi walipokuwa wakiwazuia waandamanaji kuelekea katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Mombasa kilicho umbali wa karibu mita 100 kutoka shuleni humo.

Duru katika shule hiyo zilizoomba kutotajwa jina kwa kukosa mamlaka ya kuzungumzia suala hilo ziliambia Taifa Leo kuwa, wanafunzi watatu walitibiwa na katika Kliniki ya Kaderboy wakaruhusiwa kurudi nyumbani huku wengine 12 wakipewa rufaa hadi Hospitali Kuu ya Mafunzo na Rufaa ya Pwani kwa matibabu zaidi.

Wanafunzi hao walikuwa wamepata matatizo ya kupumua kwa kuvuta gesi hiyo, wengine wanne walizirai lakini wakarejeshewa fahamu shuleni hapo huku wengine wakipata mshtuko.

Kikosi cha polisi wakiongozwa na Kamanda wa Polisi wa Eneo la Pwani, Bw George Seda, walitembelea shule hiyo kwa lengo la kubainisha ukweli na kupuuzilia mbali taarifa kuwa kitoa machozi kilirushwa ndani ya shule.

Kulingana na Bw Seda, polisi walilazimika kurusha kitoa machozi ili kuwatawanya waandamanaji waliotaka kutatiza masomo shuleni baada ya kuzuiwa kuelekea katika kituo cha polisi.

“Hili ndilo lililowafanya polisi kufyatua kitoa machozi kimoja ili kuwatawanya na shughuli ziendelee kama kawaida. Kilichoingia shuleni ni moshi tu,” alisema.

Bw Seda alithibitisha kuwa baadhi ya wanafunzi walipata matatizo ya kupumua lakini akasema ni wale ambao wana pumu.

Kisa hicho kilitilia kiza mwamko mpya ya maandamano ambayo yaliendelea kushuhudiwa Jumatano huku vijana waandamanaji wakivumilia mvua kubwa mjini Mombasa kuwasilisha malalamishi yao dhidi ya Mswada wa Fedha.

Kwa takriban saa nne, waandamanaji hao waliandamana kwa amani katikati ya mji wakisindikizwa na polisi, huku wakiimba kauli mbiu za kupinga Mswada huo huku wakipeperusha mabango na kuonya kwamba ajenda yao inayofuata itakuwa kuwarejesha nyumbani Wabunge kwa kushindwa kuwatetea wananchi.

Maandamano hayo yaliyopewa jina la ‘OccupyMombasa’ ambayo yaliratibiwa kupitia mitandao ya kijamii ikiwa ni pamoja na WhatsApp, X na TikTok yalifanyika siku moja baada ya maandamano sawia kufanyika jijini Nairobi.

Waandamanaji hawakushirikisha viongozi wa kisiasa wala wahuni ambao kwa kawaida hulaumiwa kwa kusababisha uharibifu na wizi wakati wa maandamano.

Karibu na eneo la ‘Pembe za Ndovu’

Waandamanaji walikuwa wameanza kukusanyika kwenye eneo la ‘pembe za ndovu’ kando ya barabara ya Moi Avenue saa mbili asubuhi. Kufikia saa tatu asubuhi, idadi ya maafisa wa polisi walikuwa wamewasili kujaribu kusimamisha maandamano.

Jaribio la awali la vijana hao kutaka kuandamana lilizimwa na maafisa wa polisi ambao walisema hawana kibali na kuwafyatulia vitoa machozi ili kuwatawanya.

“Ukitaka kuandamana lazima ulete barua. Mimi ndiye OCS na sijapokea barua yoyote kutoka kwenu, kwa hivyo hakutakuwa na maandamano,” afisa mkuu wa polisi wa kituo cha Central, Bw Peter Mugambi alisema.

Hata hivyo, Bw Mugambi baadaye aliruhusu maandamano hayo kuendelea kwa amani, akiwataka waandamanaji kufanya hivyo kimyakimya.

Waandamanaji walisema wameamua kujitokeza wakiwa vijana wa Kenya na kuwaonya Wabunge kuwa waangalifu kwani watapanga pia kuwarejesha nyumbani baadhi yao kwa kushindwa kutetea haki za wananchi.

“Natumai wabunge wetu wametusikia. Hatutasubiri hadi 2027, tutawaondoa. Kwa wale wasiojua kuwaondoa wabunge mamlakani, sisi ni vijana. Tutawafundisha,” Mary Gachuri, mwandamanaji, alisema.

Walisisitiza kuwa wataendelea kutumia haki zao za kidemokrasia bila woga.

Bi Juliey Mumia, msanii anayeishi Mombasa, alisema umma hauwezi tena jinsi gharama ya maisha inavyopanda kupita kiasi.

“Tunakataa Mswada mzima wa Fedha. Maisha ni ghali sana, hatuwezi kumudu kupanda kwa bei ya bidhaa,” alisema.

Maoni sawa na hayo yalitolewa na Bw Clinch Ondege, ambaye alilalamikia hali ya ufadhili wa afya nchini.

“Ninakataa Mswada wa Fedha kwa sababu ya kupunguzwa kwa bajeti ya afya ya uzazi na huduma ya uzazi,” akasema.

Kwa upande wake, msanii wa muziki wa hip hop kutoka Pwani, Mohamed Kesi almaarufu Kaa la Moto, alitoa wito kwa wenzake katika tasnia hiyo kuungana na maandamano yanayoendelea, akisema mambo yaliyopo yatawaathiri pia moja kwa moja.

“Toka nje ya studio, jiunge na vijana hawa wa Kenya kupigania maisha yetu. Mombasa imeonyesha nchi nzima kuwa hufai kupigana katika maandamano ili ujumbe wako usikike,” akasema.

Bw Tom Odipo, mwanafunzi kutoka Mombasa, alihimiza umma kusoma Mswada uliopendekezwa na kutambua kilicho hatarini. Hakuna walioripotiwa kukamatwa kwenye maandamano hayo ambayo yalitamatika mwendo wa saa saba mchana, wakati waandamanaji walitawanyika wenyewe.