Habari Mseto

Mwizi wa njugu karanga ahukumiwa kifungo cha nje miaka miwili

June 11th, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

KIBARUA aliyeiba kilo 15 za njugu karanga kuziuza apate nauli kusafiri hadi mashambani kumwona na kumpeleka mama yake mgonjwa hospitalini, amehukumiwa kutumikia kifungo cha nje kwa kipindi cha miaka miwili.

Akimhukumu Daniel Mukhwana, Hakimu Mwandamizi mahakama ya Milimani Ben Mark Ekhubi alisema Jumanne kwamba mshtakiwa alijutia makosa yake na akaahidi kutorudia makosa hayo.

“Nimetathmini ripoti ya afisa wa urekebishaji tabia kwamba mshtakiwa amejutia makosa yake,” alisema Bw Ekhubi.

Hakimu alisema watu wa familia ya mshtakiwa na naibu chifu walieleza kwamba mshtakiwa hakuwa na rekodi yoyote ya kushiriki uhalifu.

Pia ripoti ya urekebishaji tabia ilisema kwamba mshtakiwa ni msikivu na mtiifu na kwamba “yuko tayari kubadili mwenendo wake”.

“Hii mahakama imetilia maanani ripoti ya afisa wa urekebishaji tabia na pendekezo kwamba mshtakiwa anastahili kupewa fursa ya kujirekebisha. Hivyo basi, naamuru mshtakiwa atumikie kifungo cha nje cha miaka miwili,” aliamuru Bw Ekhubi.

Hakimu alimtaka Mukhwana kushirikiana na maafisa wa urekebishaji tabia pamoja na kujiepusha na visa vya uhalifu.

“Ikiwa utashiriki uhalifu na kufikishwa hapa kortini tena kabla ya kukamilisha kifungo hiki cha miaka miwili, hii mahakama itafutilia mbali kifungo hiki kisha utumikie kifungo cha jela,” hakimu alimuonya mshtakiwa.

Mukhwana alikiri kuiba kilo 15 za njugu karanga za thamani ya Sh6,000 katika soko la Tsunami lililoko jijini Nairobi.

Akijitetea alieleza mahakama ya Milimani kwamba aliiba njugu hizo auze apate nauli ya kuenda nyumbani kumpeleka mama yake mzazi hospitalini.

Aliomba korti imsamehe kisha imwachilie huru akampeleke mama yake kwa matibabu.

Mukhwana aliungama mbele ya Bw Ekhubi kwamba aliiba njugu karanga zenye thamani ya Sh6,000.

Alipoulizwa na Bw Ekhubi sababu za kuiba njugu hizo, Mukhwana alijieleza.

“Ni ukweli niliiba njugu karanga kutoka kwa duka la Bi Jane Wanjiru Mburu ninayemfanyia kazi ya kuzikaanga kwa karai nikitumia makaa,” Mukhwana aliungama.

Bw Ekhubi alimwuliza mshtakiwa, “Ni sababu gani iliyokufanya uibe njugu hizi?”

Akajibu Mukhwana, “Mheshimiwa, niliiba hizi njugu kuziuza nipate nauli kusafiri hadi mashambani kumwona mama yangu ambaye ni mgonjwa. Yapata mwezi mmoja tangu augue. Nilipokea simu kwamba mama yangu mzazi ni mgonjwa sana na sina pesa za kulipa nauli niende kumwona.”

Mshtakiwa huyo alisema hana pesa kutokana na hali ngumu ya kiuchumi ambayo imemfanya aishi maisha ya uchochole.

“Madaktari wamekuwa wamegoma na mama yangu ameumia bila kupata msaada wa kimatibabu. Nilikuwa nataka niuze hizi njugu karanga nipate nauli ya kusafiri hadi nyumbani kisha nimpeleke katika kliniki ya kibinafsi,” Mukhwana aliungama akijitetea.