Afya na Jamii

Namna ya kukabili tatizo la harufu mbaya kinywani

May 13th, 2024 2 min read

NA PAULINE ONGAJI

TATIZO la harufu mbaya mdomoni au halitosis, laweza kusababishwa na bakteria ya kinywani. Yaweza kuwa pia kutokana na maradhi ya ufizi au masalio ya chakula kinywani.

Wataalamu wa meno wanasema kwamba unapaswa kupiga mswaki na kuondoa masalio ya chakula kwa kutumia uzi maalum wa hariri (floss) kila baada ya kula angalau mara mbili kwa siku, na pia usugue ulimi wako.

Vilevile, unaweza kutumia dawa maalumu ya mdomoni kusukutua kila baada ya kusugua meno. Pia, unashauriwa kukaguliwa na daktari wa meno ili yasafishwe na uchafu uondolewe kwani uchafu huu huchangia meno kuoza na harufu mbaya mdomoni.

Lakini pia, chakula unachokula kwa wingi kina uwezo wa kuchochea hali hii. Kwa mfano, vyakula kama vile vitunguu na vitunguu saumu, baadhi ya viungo na samaki, vimethibitishwa kuchochea hali hii.

Aidha, kula vyakula vyenye viwango vya chini vya wanga, kwa mfano wakati wa mfungo, vyaweza sababisha mwili kuyeyusha mafuta mwilini na hivyo kusababisha uzalishaji wa kemikali aina ya ketones, ambazo husababisha harufu inayokaribiana na ile ya matunda unapopumua.

Ili kukabiliana na tatizo hili, mbali na kuzingatia usafi na afya ya kinywa, kuna vyakula ambavyo ukivila, vitakusaidia kukabiliana na tatizo hili.

Kwa mfano, mboga na matunda kama vile pea, karoti na tufaha husaidia kuzalisha mate mdomoni na hatua hii husaidia kusafisha bakteria inayosababisha harufu mbaya kinywani.

Aidha, mboga na matunda haya yana viwango vya juu vya nyuzi na hivyo husaidia kuondoa uchafu kwenye meno unavyoendelea kula.

Pia, matunda kama vile machungwa, yana viwango vya juu vya virutubishi vya vitamini C ambavyo husaidia kuzuia kishuzishuzi.

Aidha, matunda ya cheri huondoa harufu ya gesi ya methyl mercaptan inayopatikana katika vyakula kama vile vitunguu na baadhi ya chizi, ambazo husababisha harufu mbaya mdomoni.

Mbali na hayo, viungo vya katekini (catechins) na kemikali asili za kusafisha mwili zinazopatikana kwa wingi kwenye chai ya kijani, zaweza kusaidia kukabili tatizo la harufu mbaya kinywani.

Kiungo cha tangawizi kwa upande mwingine kina kemikali maalum iitwayo 6-gingerol ambayo huchochea uzalishaji wa kimeng’enyo maalum kwenye mate ambacho huvunja vunja kemikali ya salfa mdomoni.

Vilevile, kotimiri na mrihani, zina kemikali asili za polyphenols, ambazo husaidia kuondoa harufu mbaya kinywani.