Habari za Kitaifa

Ng’o, hatutakubali upunguze mgao wa kaunti, maseneta waambia Ruto

Na COLLINS OMULO July 1st, 2024 2 min read

RAIS William Ruto anakabiliwa na kizingiti kikubwa katika juhudi zake mpya za kupunguza matumizi kuziba pengo la bajeti la Sh346 bilioni huku maseneta wakiapa kukataa kupunguzwa kwa pesa za mgao wa kaunti.

Rais alitangaza wiki jana kwamba pendekezo la kupunguza matumizi litatekelezwa kwa usawa na serikali za kitaifa na zile za kaunti.

Haya yalijiri baada ya kiongozi wa nchi kukataa kuidhinisha Mswada tata wa Fedha wa 2024 ambao ungefanya serikali ya kitaifa kuongeza mapato ya ndani kwa Sh346 bilioni.

“Nimerejesha Mswada wa Ugavi wa Mapato wa Kaunti, ambao ulitegemewa kutoka kwa Mswada wa Fedha uliokataliwa, kurudi Bungeni ili kupunguzwa ipasavyo,” alisema Rais Ruto.

Rais pia aliiagiza Hazina ya Kitaifa kuwasilisha mara moja Bungeni marekebisho ya Sheria ya Mgao wa Mapato ya 2024 ili kuakisi mapato yaliyopunguzwa baada ya kukataa kutia saini Mswada wa Fedha kuwa sheria.

Hata hivyo, maseneta wamemuonya Rais kutoingilia mgao wa Sh400.1 bilioni wa mapato uliotengewa kaunti 47 kama sehemu ya hatua zake za kupunguza matumizi.

Kiongozi wa Wachache katika Seneti Ledama Olekina alitaja tangazo hilo la Rais kuwa ‘upumbavu,’ akirejelea sehemu ya 5 ya Sheria ya Mgao wa Mapato.

Seneta huyo wa Narok alisema ni serikali ya kitaifa inayofaa kubeba upungufu wowote wa mapato na wala sio serikali za kaunti.

Kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Mgao wa Mapato kinasema iwapo mapato halisi yanayopatikana kitaifa katika mwaka wa fedha yatapungua kuliko mapato yaliyotarajiwa, nakisi hiyo itabebwa na serikali ya kitaifa.

“Ni rahisi hivyo. Hatutaki chochote cha kaunti kuguswa. Yeyote anayemshauri hana habari. Muache alenge burudani, ukarabati na bajeti zake za siri katika afisi yake na aache kaunti,” akasema Bw Olekina.

Alimlaumu Rais kwa kutaka kuchukua kazi ya bunge ya kutunga sheria.

“Pesa hizo tayari zilikuwa zimegawanywa kati ya serikali ya kitaifa na ya kaunti na hakuna jinsi tutaanza mchakato mwingine mpya,” alisema.

Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na naibu kinara wa wachache katika Seneti walisema hawataunga mkono kupunguzwa kwa pesa za kaunti.

Alisema kuwa Seneti, waliidhinisha Sh415 bilioni kutumiwa kwa kaunti lakini ni Sh400.1 bilioni pekee ndizo zilizokubaliwa.

“Hatutaachilia senti yoyote kutoka kwa Sh400 bilioni. Hatua za kupunguza matumizi zinahusu serikali kuu. Kaunti zina asilimia 10 pekee ya bajeti kinyume na asilimia 90 ya serikali ya kitaifa. Wakenya wanaposema acha ufujaji serikalini, hawazungumzii kaunti bali serikali ya kitaifa. Alenge afisi yake,” Bw Sifuna aliongeza.

Mswada wa Ugavi wa Mapato wa Kaunti, 2024 kwa sasa uko katika hatua ya pili ya kusomwa katika Seneti.

Walipokuwa wakijadili mswada huo, maseneta waliomba serikali ya kitaifa kusambaza fedha zaidi kwa kaunti.

Seneta wa Machakos Agnes Kavindu kaunti bado zinakabiliwa na changamoto nyingi  hospitali kwa sababu ya uhaba wa pesa.

“Kaunti zinawalipa madaktari, kununua dawa, kujenga hospitali mpya hapa na pale na mambo mengine mengi. Fedha hazitoshi. Ninaomba Serikali ya kitaifa ipeleke pesa zaidi za afya na kilimo kwa kaunti, ili tufanye kazi bila kutatizika,” akasema Bi Agnes.

Seneta wa Nandi Samson Cherargei alisema kaunti zinafaa kupata takriban Sh500 bilioni kukidhi shughuli zilizogatuliwa.