Habari za Kitaifa

Ni kuchezwa? Azimio wadai mswada ulioletwa Bungeni bado una ushuru ‘uliofutwa’


WITO wa kudumisha shinikizo za kisiasa ili mabadiliko zaidi yafanyiwe Mswada wa Fedha wa 2024 ni miongoni mwa sababu zilizofanya upinzani kukataa kuidhinisha mageuzi ya serikali katika mswada uliopendekezwa.

Katika mkutano uliochukua takriban dakika 90 katika County Hall Jumanne jioni, muungano wa Azimio la Umoja ulisema kwamba kuunga mkono Mswada huo kulingana na mabadiliko yaliyotangazwa Ikulu, kungekuwa kumeza chambo cha kisiasa cha Rais Ruto kutaka waunge mapendekezo mengine yaliyomo kwenye Mswada ambao bado wanasema ni hatari.

Taifa Leo pia imefahamu kuwa muungano huo umeitisha mkutano mwingine leo jioni ili kuafikiana kuhusu marekebisho ya jumla utakaoshinikiza katika Mswada huo.

Kiranja wa wachache katika Bunge la Kitaifa Junet Mohammed alithibitisha kuwa wabunge hao walikubaliana kuwa na mkutano mwingine wa wabunge ili kuweka mikakati ya marekebisho yatakayofanywa wakati wa kikao cha Bunge zima.

“Baadhi ya wabunge walikuwa na maoni kwamba tusipendekeze marekebisho yoyote huku wengine wakisema tufanye hivyo. Kwa hivyo, tulikubali kukutana tena na kukagua jinsi mjadala umekuwa, kisha tuje na marekebisho ya pamoja ili kushinikiza mabadiliko zaidi,” Bw Mohamed aliambia Taifa Leo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Uhasibu (PAC) John Mbadi alisema muungano huo bado unapinga Mswada huo kwa kuwa sheria ni mchakato unaofanywa Bungeni na si tukio linalofanyika Ikulu.

“Tunapozungumza, Mswada umesomwa kwa mara ya kwanza. Unakuja mara ya pili na bado una vifungu hatari. Hatuwezi kukubali matamshi yanayotolewa katika Ikulu,” Mbadi alisema.

“Hadi mapendekezo hayo yatakapopitishwa na Bunge, bado tunapinga Mswada huo.Tunataka Mswada huo uondolewe kabisa kwani bado kuna vipengele vya kuumiza raia,” Bw Mbadi alisema.

“Rais Ruto alibanwa tu na Wakenya, hamfanyii yeyote hisani katika kutupilia mbali vipengele vya kuumiza raia,” alihoji.

Jana bungeni mbunge wa Seme, James Nyikal aliibua masuala kuhusu jinsi Mswada huo ulivyowasilishwa, akieleza kuwa Ikulu tayari imejadili ripoti ya kamati na hata kupendekeza mabadiliko yake hata kabla ya kuwasilishwa Bungeni kama ulivyo utaratibu.

“Ripoti hii ilienda kwa Rais kabla haijatujia. Tumekiuka kanuni na hivyo mtu yeyote anaweza kutumia mahakamani kupinga Mswada huu ukishapitishwa. Utaratibu unafaa kuwa kwamba bunge likamilishe kazi yake, kisha upeleke kwa rais badala ya kupelekwa huko kwanza,” Dk Nyikal alisema.

Hata hivyo spika Moses Wetang’ula alisema bunge wanaruhusiwa kukutana kujadili masuala na hata upande wa Azimio ulikuwa na mkutano kujadili ripoti hiyo.

Mnamo Jumanne, utawala wa Rais Ruto ulikubali shinikizo la umma na kuondoa baadhi ya ushuru dhalimu ambao ulikuwa umependekezwa katika Mswada huo.