Habari Mseto

Okanga sasa ashtakiwa ‘kukosea heshima’ viongozi wa serikali


MWANAHARAKATI na mfuasi sugu wa Azimio la Umoja, aliye pia mwanafunzi wa Kidato cha Kwanza Nuru Okanga Maloba ameshtakiwa rasmi kuchapisha habari za kupotosha kuhusu maafisa wakuu serikalini.

Okanga, ambaye anasoma katika Shule ya Upili ya Mwangaza iliyoko Kayole, Nairobi amedaiwa kuandika habari za kuudhi dhidi ya Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua.

Mashtaka yanasema kwamba Okanga, katika mojawapo ya machapisho aliyotundika mitandaoni, alimtaka Bw Gachagua “kumpiga risasi Ruto”, maandishi yaliyochukuliwa kuzua uhasama, chuki, na kukosea adabu viongozi wa nchi.

Mwanafunzi huyo alidaiwa alichapisha habari hizo mnamo Juni 7 na 12, 2024 katika mtandao wake wa Riba News @ribanews kinyume cha sheria za mawasiliano.

Mwanaharakati Nuru Maloba Okanga akiwa kizimbani Juni 19, 2024. Picha|Richard Munguti

Pia alikabiliwa na kuchapisha habari za kumdharau Rais Ruto kwa kumtaka “rubani anayeendesha ndege inayombeba rais adungwe shindano.”

Mawakili Shadrack Wambui na Kevin Onani waliomba mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana wakisema “hana pesa, anawategemea wafadhili kumlipia karo ya shule na kujikimu kimaisha.”

Bw Wambui alidokeza kwamba mshtakiwa ameoa na wamejaliwa kupata mtoto mmoja.

“Mshtakiwa huyu ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza. Ameoa. Mkewe anaugua na mtoto wao amelazwa katika Hospitali Kuu ya Kenyatta. Naomba aachiliwe kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu,” Bw Wambui alisema.

Kiongozi wa mashtaka James Gachoka hakupinga ombi hilo la dhamana.

Bw Ochoi alimwamuru Okanga alipe dhamana ya pesa tasilimu Sh100,000 afanye kesi akiwa nje.

Kesi hiyo itatajwa Julai 3, 2024 kwa maagizo zaidi.