Siasa

Serikali yaweka mikakati ya kumzolea Raila kiti cha AUC

June 5th, 2024 1 min read

NA JUSTUS OCHIENG

SERIKALI ya Kenya Kwanza imeweka mikakati ya kuhakikisha kiongozi wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga anapata kura za kumwezesha kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Masuala ya Kigeni, alisema Jumatano kwamba Bw Odinga ana tajriba pevu inayoweza kusaidia kuleta mageuzi yanayohitajika katika AUC.

“Tuna kiongozi mwenye maono wa kuleta mageuzi muhimu katika Umoja wa Afrika (AU). Bila shaka atalenga kupata mafanikio yanayoendana na matarajio ya mataifa ya bara Afrika. Kufikia sasa, mgombea wetu ameonyesha uwezo mkubwa wa kuibuka mshindi,” akasema Bw Mudavadi.

Kwa upande wake, Bw Odinga ametoa hakikisho kwamba akipata kazi hiyo, atashauri mataifa ya Afrika kuimarisha ushirikiano kuanzia kwa ukuaji wa kiuchumi hadi mtandao wa uchukuzi na usafiri.

“Ukienda Ulaya, mtu anahitaji kibali kimoja kusafiri kutoka kwa taifa moja kuenda mataifa mengine yote ya Muungano wa Ulaya (EU). Huku kwetu ukitoka Kenya kuenda Tanzania unahitaji kibali… ukitoka Tanzania kuenda Malawi unahitaji kibali kingine,” akasema Bw Odinga.

Kiongozi huyo wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) alisema kiti anacholenga ni cha bara la Afrika na wala si cha kisiasa nchini.

“Nilishauriwa na marafiki wengi wa kutoka nje kuwania kiti hiki. Serikali inaniunga mkono kwa sababu uwaniaji wangu ni wetu sote Wakenya… si wa chama fulani,” akasema.