Habari Mseto

Uhalifu sasa warejea kwa kishindo katika eneo la Likoni

March 18th, 2019 2 min read

Na HAMISI NGOWA

HALI ya utovu wa usalama imeanza kushuhudiwa tena katika eneo la Likoni Kaunti ya Mombasa, licha ya maafisa wa polisi kudhibiti hali katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Wakazi katika eneo hili walifurahia hali ya usalama tangu mwezi Disemba mwaka uliopita lakini katika kipindi cha siku tatu zilizopita hali imekuwa si hali tena katika baadhi ya mitaa eneo hilo.

Magenge ya vijana wahalifu yameanza kuchipuka upya na kuanza kulitikisa eneo hili kwa kuwahangaisha wakazi katika baadhi ya mitaa.

Mashambulizi hayo yameanza kuzua hofu miongoni mwa wakazi baada ya mtu mmoja kupoteza maisha akipelekwa hospitalini huku wengine watatu wakijeruhiwa katika visa vitatu tofauti.

Kisa cha kwanza kilitokea siku ya Jumatano katika mtaa wa Jamvi la Wageni ambapo mwanamume wa umri wa miaka 27 alishambuliwa na genge la wahalifu na kupoteza maisha yake wakati alipokuwa akikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa kwa matibabu.

Marehemu anayefanya kazi ya ulinzi katika kampuni moja ya kibinafsi alikumbana na genge la vijana ambao idadi yao haikuweza kujulikana wakati alipokuwa akielekea kazini majira ya saa kumi na nusu alfajiri.

Kisa cha pili kilifanyika katika mtaa wa Nuru siku ya Alhamisi majira ya saa tatu usiku ambapo mwanamume mwingine alishambuliwa kwa mapanga na genge la vijana zaidi ya watano.

Mwathiriwa huyo alikuwa akitoka kazini akielekea nyumbani wakati alipovamiwa. Alipokonywa simu ya mkononi pamoja na pochi yake ambayo ilikuwa na pesa pamoja na stakabadhi zake nyingine.

Katika kisa hicho, mwathiriwa huyo alijeruhiwa baada ya kukatwa sehemu ya kichwani pamoja na sikio la kulia wakati alipojaribu kukabiliana na genge hilo.

Kisa cha tatu nacho kilitokea jana Ijumaa saa mbili asubuhi katika mtaa wa Jamvi la Wageni ambapo genge la vijana watano wenye silaha butu pamoja na visu na panga walimshambulia mwanamume na kumjeruhi.

Mwathiriwa ambaye alikuwa akielekea kazini, alisema kuwa mmoja wa vijana hao aliyekuwa amejihami kwa kisu alitokea nyuma na kupita mbele yake ambapo alijaribu kumshambulia lakini wakati alipojaribu kumkabili,alishambuliwa kwa nyuma na wengine waliokuwa na mapanga.

“Nilikuwa njiani nikielekea kazini Fort Jesus wakati nilipovamiwa na kushambuliwa na vijana. Mimi ni mgeni katika sehemu hii. Nimeishi hapa kwa wiki tatu pekee. Naishi kwa binamu yangu aliyenitafutia kazi,”akaeleza.

Hata hivyo, alisema baada ya tukio hilo alibebwa na wasamaria wema hadi katika kituo cha polisi cha Likoni ambapo walishauriwa wamepeleke katika Hospitali ya Likoni kwa matibabu.

Anasema baada ya kufikishwa hospitalini aliachwa nje kwa muda bila ya kuhudumiwa kwasababu ya kukosa pesa hadi mtu mmoja msamaria mwema alipojitolea kulipia gharama za matibabu yake.

“Polisi walituambia tuje hapa kwa kuwa ndiyo Hospitali ya serikali inayotoa huduma za bure za matibabu lakini tulipofika tukapata mambo ni tofauti,’’ akasema.

Kaimu afisa mkuu wa upelelezi katika eneo hilo Bw Charles Onyango amesema kwamba washukiwa watatu wametiwa mbaroni na wanawasaidia maafisa wa usalama katika uchunguzi.