Habari za Kitaifa

Wabunge walivyokunja mkia kuhusu kujiongeza mshahara kama walivyozoea

Na ALEX NDEGWA July 5th, 2024 2 min read

KWA mara ya kwanza nchini, wabunge wamejitokeza hadharani kukataa nyongeza ya mishahara huku wakishutumu Tume ya Mishahara (SRC) kwa kuchochea uhasama baina yao na umma.

Haya yamejiri kufuatia maandamano ambayo yamekuwa yakiendeshwa na vijana almaarufu Gen Z kote nchini kupinga Mswada wa Fedha 2024, ambayo yamewaingiza baridi wabunge.

Kulingana na notisi iliyochapishwa na Tume ya Mishahara (SRC) wabunge wote 349 na Seneti 67, wangepata nyongeza isiyopungua Sh14,000 kila mmoja kuanzia Julai 1.

Hata hivyo, serikali imelazimika kusitisha utekelezaji wa Notisi Rasmi ya Agosti 9, 2023, ambapo SRC iliorodhesha mishahara na marupurupu ya maafisa wa serikali katika bajeti iliyoanzia 2021/2022 hadi 2024/2025.

Ripoti ya SRC kuhusu Awamu ya Tatu ya Mishahara na Marupurupu ilizidisha ghadhabu ya Wakenya ambao wamekuwa wakiandamana kote nchini kulalamikia gharama ya juu ya maisha.

Mbunge wa Emabaksi Mashariki, Babu Owino ni miongoni mwa walioghairi nia hiyo huku akitaja hatua ya SRC kama isiyofaa wakati huu ambapo taifa limelemewa kifedha.

“Wabunge na maafisa wa serikali hawafai kuongezwa hata senti. Inahuzunisha kuongeza mshahara wakati Wakenya hawana kazi, Wakenya hawana mtaji wa kuanzisha biashara, Wakenya hawana karo ya shule wala pesa za matibabu sembuse pesa za nyongeza ya mishahara!,” alisema Bw Owino kupitia mtandao wa kijamii wa X.

Mzigo kwa mlipa ushuru

Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Aaron Cheruiyot alisema SRC imekuwa kimya wakati wa maandamano na kuitaka Tume hiyo kuvunja kimya chake kuhusu namna ya kupunguza mzigo wa mishahara kutoka asilimia 46 hadi kiasi kiasi kinachohitajika cha asilimia 35 ya mapato kitaifa.

“Ikiwa inamaanisha kukatwa mishahara, sisi kama wabunge tumeambiwa kamwe hatuna chaguo jingine. Hatuna hiari, ni sharti tufanye hivyo,” alisema Seneta Cheruiyot.

Mwezi mmoja tu baada ya kuchaguliwa Bungeni baada ya Uchaguzi Mkuu Agosti 9, 2022, wabunge walianza kulalamikia pendekezo la SRC kuhusu kuwapunguzia mishahara.

Ilijumuisha kuondoa Sh5,000 za marupurupu ya kuhudhuria vikao vya Kamati, hatua ambayo SRC ilisema ingeokoa Sh1 bilioni kila mwaka.

Kudhibiti ukubwa wa injini za magari ya wabunge yanayogharimiwa na walipa ushuru ikiwa ni pamoja na kupunguza masafa ya usafiri.

SRC ilichapisha mabadiliko haya katika Notisi Rasmi kabla ya uchaguzi Julai 28, ambapo vilevile yalilenga kupunguza idadi ya wanandoa na watoto ambao mbunge anaweza kujumuisha katika bima ya matibabu inayofadhiliwa na serikai ili kuzuia wabunge wanaoitumia vibaya kupitia mipango ya kando.

Mageuzi hayo yalisababisha wabunge wapya kuorodhesha mstari wa mbele suala la nyongeza ya mshahara huku wakimkabili vikali Mwenyekiti wa SRC, Lyn Mengich.

Septemba 21,2022, Bi Mengich, alihojiwa kwa saa sita na wabunge waliojawa na hamaki.