• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
Mshahara wa Sanchez unavyozidi kuzua tumbo joto Trafford

Mshahara wa Sanchez unavyozidi kuzua tumbo joto Trafford

Na CHRIS ADUNGO

MSHAHARA wa Alexis Sanchez kambini mwa Manchester United umeshuhudia gharama ya matumizi ya kikosi hicho ikiongezeka kwa asilimia 10.

Haya ni kwa mujibu wa rekodi mpya za fedha zilizotolewa na miamba hao wa soka ya Uingereza.

Fowadi huyo mzawa wa Chile kwa sasa anapokea kima cha Sh42 milioni kwa wiki, ujira ambao umekadiriwa kufikia hadi Sh70 milioni kwa wiki bonasi na marupurupu ya kila mwezi yakijumuishwa.

Kutokana na ujio wa Sanchez ugani Old Trafford akitokea Arsenal mwanzoni mwa Januari 2018, klabu ya Man-United ilijipata katika ulazima wa kuwalipa wachezaji wake mshahara wa zaidi ya Sh10 bilioni kufikia mwisho wa Septemba 2018.

Kiasi hiki cha fedha ni ongezeko la asilimia 10.2 la gharama ya matumizi ya Man-United kwa mwaka.

Kulingana na kikosi hicho, huenda matumizi hayo yakaongezeka hata zaidi iwapo usimamizi utashawishika kuongeza mshahara wa kipa David de Gea ambaye ametoa masharti mapya kwa waajiri wake hao.

Kipa huyo mzawa wa Uhispania mwenye umri wa miaka 27 ametishia kubanduka Old Trafford mwisho wa msimu huu iwapo miamba hao hawataongeza ujira wake hadi ukaribiane na ule wa Sanchez, sogora ambaye kwa sasa anadumishwa kwa mshahara mkubwa zaidi katika soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

De Gea amekuwa windo la Real Madrid kwa muda mrefu, japo kwa sasa haijulikani anakolenga kuyoyomea baada ya wafalme hao wa Uhispania kujinasia huduma za aliyekuwa mlinda-lango wa Chelsea, Thibaut Courtois.

Kwa mujibu wa wadadisi wengi wa soka ya EPL, kusajiliwa kwa Sanchez ndicho kiini cha msukosuko uliotishia kulemaza kabisa makali ya Man-United katika kipindi cha kuanzia mwisho wa msimu jana hadi sasa.

Mshahara wa Sanchez ulivuruga Amani ya Paul Pogba, kiungo ambaye hadi ujio wa Sanchez, alikuwa ndiye mchezaji ghali zaidi Trafford.

Kimshahara, migongo ya wawili hao kwa sasa inasomwa na Romelu Lukaku na De Gea wanaokula Sh28 milioni kila mmoja kwa wiki.

Mbali na unono wa mishahara ya wachezaji hawa, kingine kilichopaliza gharama ya matumizi ya Man-United ni kusajiliwa kwa wachezaji Fred, Diogo Dalot na Lee Grant. Kurefushwa kwa mkataba wa kiungo Marouane Fellaini ni sabau nyingine.

Licha ya kuwa mchezaji anayelipwa mshahara wa juu zaidi, mchango wa Sanchez kambini mwa Man-United ni mdogo sana huku ushawishi wake ukikosa kabisa kuhisika ugani.

Kufikia sasa, nyota huyo wa zamani wa Barcelona amewafungia Man-United mabao manne pekee kutokana na mechi 29 zilizopita.

Sanchez amesazwa nje ya kikosi cha kwanza cha Man-United katika michuano minne ya EPL.

Hilo limemchochea kocha Jose Mourinho kuanza kumwondoa Sanchez katika mipango ya baadaye ya Man-United hasa ikizingatiwa kwamba kwa sasa ni miongoni mwa wachezaji wanaokamilisha kikosi cha akiba hata katika michuano ya haiba kubwa.

Mwanzo mbaya katika maisha ya Sanchez uwanjani Old Trafford kwa sasa umeibua tetesi zinazomhusisha na uwezekano wa kuagana na Man-United.

Iwapo atavunja uhusiano wake na kikosi hicho, basi atakuwa mchezaji wa kwanza wa haiba kubwa kuagana na Man-United baada ya kipindi cha chini ya mwaka mmoja.

Huduma za mvamizi huyo ambaye pia amewahi kuvalia jezi za Udinese nchini Italia, tayari zinahemewa na Paris Saint-Germain (PSG) huku maarifa yake yakimezewa mate na Real Madrid na Bayern Munich vilevile.

You can share this post!

2022: Mbinu mpya ya Raila kuzoa kura za Mlima Kenya

JAMVI: Kalonzo alijikwaa kisiasa kukubali kuwa ‘mtu wa...

adminleo