Makala

Gen Z waanza ‘kuaga maandamano’ wahuni wakijitosa uwanjani


MAANDAMANO yanayoendelea dhidi ya serikali yameanza kupoa huku visa vya wahuni kuiba mali na kusababisha uharibifu vikikithiri.

Japo maandamano yanaendelea, hayajafikia uzito wa yaliyoshuhudiwa juma lililopita.

Vijana wanaopiga parapanda mitandaoni kumshinikiza Rais William Ruto ajiuzulu, wameanza kuwaambia wenzao wasitishe kuandamana na badala yake kuelekea nyumbani wasihusishwe na uhuni.

“Tulisema hakuna kutumia mawe, ni simu tu. Hao walio barabarani ni wahuni. Nendeni nyumbani kiza kisiwapate nje,” alisema, Osama Otero, mtumiaji mitandao ya kijamii ambaye amekuwa mstari wa mbele kupinga utawala wa serikali ya Kenya Kwanza.

“Kaeni chonjo kuna wahuni na wezi katikati ya jiji ambao wanajifanya waandamanaji wa Gen Z. Ukiwaona, wapige picha…kuna mtu anaweza kumtambua mmoja wao,” Bw Billy Simani, maarufu Crazy Nairobian, aliandika kwenye mtandao wa X.

Vijana wa kizazi cha Gen Z walianzisha maandamano ya amani majuma mawili yaliyopita kupinga kuidhinishwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024.

Lakini hali ilivyo, maandamano haya yameishia kusababisha vifo vya watu 39. Wanabiashara jijini Nairobi wanasema maandamano hayo yamechochea uharibifu wa mali zaidi ya Sh3 bilioni.

Juma lililopita, Rais William Ruto alitangaza kuwa hasara zilizoshuhudiwa ni za kima cha Sh2.4 bilioni.

Baada ya Rais kusalimu amri na kuondoa mswada huo wa fedha, maandamano yaliyoshika kasi katika kaunti 36 yanaonekana kuanza kufifia.

Uchunguzi wa Taifa Leo sehemu kadhaa katikati ya jiji la Nairobi awali ulionyesha hali ya utulivu huku biashara nyingi zikifungwa na watu wachache wakionekana mitaani.

Hata hivyo, barabara katika eneo la Odeon zilijaa waandamanaji waliokuwa wakishinikiza Rais Ruto ajiuzulu. Baadhi yao walikamatwa katika mbio za paka na panya na polisi.

Sawa na vijana wengine, mwanaharakati Boniface Mwangi amewaomba waandamanaji wa Gen Z waondoke barabarani akilaumu serikali kwa ongezeko la wahuni wanaoiba, kuharibu mali na kushambulia waandamanaji.

“Tuendeni nyumbani. Kama kawaida, serikali imekubali wahuni watawale, waibe na kuteketeza mali tena. Wahuni hao wanalindwa na serikali huku waandamanaji wasiozua fujo wakipigwa, kukamatwa na hata kuuliwa. Ni aibu mambo yamegeuka kuwa hivi. Kama serikali itakuwa na tabia za kihuni, tunajiondoa,” aliandika Bw Mwangi kwenye akaunti yake ya mtandao wa X.