Shangazi Akujibu

Jembe lake halichoki, kila wakati limo shambani linalima!

May 29th, 2024 1 min read

Shangazi;

Mume wangu ana hamu ya kustaajabisha kimahaba. Anataka tendo la ndoa kila wakati. Amekuwa hata akijifanya anakuja nyumbani kula chakula cha mchana kumbe ni ngono tu anataka.

Kama mke unapaswa kumlisha mumeo upande huo. Jaribu kuzungumza naye kuhusu linalokutatiza, japo kamwe usipuuze mahitaji yake, la sivyo atapata chakula kwingine.

Mke wangu anapenda anasa kupindukia

Katika siku za hivi majuzi mke wangu amekuwa na tabia mbovu. Anatoweka Ijumaa anarejea Jumapili huku akiwa amelewa. Haambiliki na sasa naishiwa na subira. Nimtaliki?

Bila shaka hayo ni makosa lakini kabla ya kuchukua hatua hiyo kali, zungumza naye. Huenda kuna jambo linamsumbua.

Hapendi kutangamana na jamaa zangu

Shangazi, tangu nimuoe mke wangu hajawahi kupenda jamaa zangu. Hataki jamaa zangu ilhali wake wamejaza nyumba. Mambo yalivyo nafikiria kuoa mke wa pili.

Anayofanya mkeo ni makosa kwani jamaa kutoka pande zote mbili wanapaswa kukaribishwa nyumbani kwenu. Hata hivyo sidhani suluhu ni talaka. Jaribu kuzungumza naye.

Mke anadai mamangu ni mchawi, nifanyeje?

Tumeoana na mke wangu kwa miaka kumi sasa na kujaliwa watoto watatu. Majuzi mke wangu alijifungua mtoto wetu wa nne lakini kwa bahati mbaya akaaga. Hii ilimsababishia mke wangu huzuni na hata msongo wa akili. Juzi nilimsikia akimtusi mama yangu mchawi na kumlaumu kwa kifo cha mtoto wetu. Nimekasirika.

Pole kwa msiba japo lazima nikuambie aliyofanya mkeo ni makosa makubwa. Mwambie mkeo amuombe mamako msamaha. Pia, mwambie lazima awe na nidhamu na mipaka anapomzungumzia mamako.