Habari za Kitaifa

Keter adai polisi walitaka kujua uhusiano wake na Uhuru na Gachagua


ALIYEKUWA Mbunge wa Nandi Hills, Alfred Keter sasa anasema kuwa alihojiwa kuhusu uhusiano wake na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais Rigathi Gachagua baada ya kukamatwa Jumapili, Juni 30, 2024.

Bw Keter, alijiwasilisha kwa Idara ya Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai, ambapo alifichua kuwa polisi walimhoji na kumuuliza ikiwa alihusika katika ulanguzi wa silaha nchini Congo.

“Nilipokamatwa, niliulizwa kuhusu uhusiano wangu na aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta na uhusiano wangu na Naibu Rais wa sasa”, Keter alisema.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo ambaye ni mkosoaji mkuu wa serikali ya Rais William Ruto alisisitiza kuwa sababu ya kukamatwa kwake ni msimamo wake kuhusu maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha wa 2024 ambayo yamekuwa yakifanyika nchini.

Alishikilia kuwa kukamatwa kwake ni mbinu ya vitisho kufuatia ukosoaji wake mkali kwa serikali hivi majuzi.

“Tufuate sheria lakini tusitishwe ili tunyamaze,” alisema.

Vile vile, Keter alishutumu serikali ya Kenya Kwanza kwa kushindwa kutimiza ahadi zake kwa watu wa Kenya ilizowapa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022.

Mbunge huyo wa zamani pia alishutumu serikali kwa kupotosha Wakenya, jambo ambalo alilitaja kuwa sababu ya kutoridhika na utawala wa Kenya Kwanza.

Kauli yake inafuatia tukio la Jumapili ambapo alitekwa nyara ghafla mbele ya mkewe na watoto.

Keter alitolewa nje ya gari lake kwa nguvu huku familia yake ikilia walipokuwa wakitoka kanisani.

Hata hivyo, baadaye Jumapili jioni DCI ilithibitisha kwamba alikamatwa kwa madai ya kuhusika na ulanguzi wa silaha na kuchochea ghasia.

Rais wakati wa mahojiano ya mezani Jumapili usiku na wahariri kutoka mashirika makuu ya habari nchini, alithibitisha zaidi kukamatwa Bw Keter akisema kuwa polisi walimkamata kufuatia kutofuata wito wa mamlaka ya kutekeleza sheria.

Mahojiano hayo yaliyoshirikisha runinga ya NTV, Citizen na KTN, Rais alikuwa na wakati mgumu kujibu maswali kuhusu jinsi polisi walikabiliana na waandamanaji.