• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 11:34 AM
Uhuru Kenyatta arudia makosa ya mlezi wake Moi katika siasa za urithi wa urais

Uhuru Kenyatta arudia makosa ya mlezi wake Moi katika siasa za urithi wa urais

NA VALENTINE OBARA

RAIS Uhuru Kenyatta, ataondoka mamlakani akiandamwa na sifa za siasa za urithi zilizomkumba mlezi wake wa siasa, marehemu Daniel arap Moi.

Ushindi wa naibu wake, Dkt William Ruto katika uchaguzi wa urais umeibua kumbukumbu za kipindi ambapo Moi alikuwa akielekea kustaafu mnamo 2002.

Kuelekea uchaguzi wa 2002, aliyekuwa naibu rais, marehemu George Saitoti, ndiye alitarajiwa kushikwa mkono na Moi ili arithi kiti cha urais baada ya kuhudumu kama makamu wa rais kwa miaka 13.

Sawa na jinsi Rais Uhuru Kenyatta alivyomruka Dkt Ruto kuelekea uchaguzi wa mwaka huu, Moi alimruka Saitoti na badala yake akamtangaza Bw Kenyatta awe mgombeaji urais kupitia kwa Chama cha KANU.

Hali hii ilisababisha pigo kubwa kwa KANU kwa kiasi ambacho chama hicho hakijafanikiwa kurudisha hadhi yake hadi leo.

Maporomoko yaliyoshuhudiwa katika chama hicho ni sawa na yale ambayo yanaendelea kukumba Jubilee kinachoongozwa na Rais Kenyatta.

Vilevile, katika uchaguzi wa 2002, KANU ilishindwa kuhifadhi kiti cha urais na badala yake, Mwai Kibaki ndiye aliibuka mshindi kupitia kwa muungano wa Narc-Kenya.

Hata hivyo, tofauti na Moi, Rais Kenyatta alianza kuonyesha mapema dalili kwamba hangemuunga mkono naibu wake kwa urais kwani Moi alisubiri hadi dakika za mwisho kutangaza msimamo kuhusu urithi wake.

Kwa upande mwingine, ishara kuwa Rais Kenyatta angemtenga naibu wake zilianza kuonekana punde baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2017 alipoweka mkataba wa maelewano na Bw Odinga.

Akizungumza Jumatatu baada ya mahakama kutoa uamuzi wake, Dkt Ruto alidai kuwa Rais Kenyatta alikuwa huru kumuunga mkono yeyote aliyemtaka kuwa mrithi wake.

“Nilipoamua kumunga mkono Uhuru Kenyatta kwa urais, sikumwekea masharti kwamba lazima aniunge mkono kwa hivyo sina kinyongo kwamba aliamua kumuunga mkono mtu mwingine. Tutaendelea kuwa marafiki vile tulivyokuwa awali na tutashirikiana kuendeleza Kenya mbele,” akasema.

Wakati wa kampeni za urais, baadhi ya wanasiasa wa mrengo wa Kenya Kwanza walimkashifu Rais Kenyatta wakisema alienda kinyume na ahadi waliyodai alimpa naibu wake, kwamba ataongoza kwa miaka kumi kisha amuunge mkono.

  • Tags

You can share this post!

Korti yathibitisha Ruto ni Rais wa 5

Ruto awanyooshea Uhuru na Raila mkono wa maridhiano

T L