Siasa

Kongamano la Limuru III laanza viongozi Mlima Kenya wakitoa kauli zao

May 17th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

KONGAMANO lililosubiriwa kwa hamu na ghamu la Limuru III hatimaye limeng’oa nanga rasmi.

Limeanza kwa maombi kutoka kwa wazee wa jamii ya Agikuyu kisha baadaye wazee wa Aembu na Ameru nao wakafanya maombi.

Mwandalizi mkuu wa kongamano hilo ni kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua huku akiungwa mkono pakubwa na aliyekuwa Gavana wa Laikipia Ndiritu Muriithi na Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni.

Mzee wa Jamii ya Agikuyu Wachira Kiago ni miongoni mwa watu mashuhuri waliohudhuria kongamano hilo la Limuru III.

Aliyekuwa Gavana wa Kiambu Bw Ferdinand Waititu alizua msisimko alipowasili saa nne na dakika 24.

Mzee Nyamu wa Njoka akihutubu kwenye kongamano hilo alisema Uchaguzi wa 2022, Mlima Kenya ulikuwa wa ukaidi na uliotenganisha wengi hata ndani ya familia.

“Tulijiangazia kama wasiojielewa na wasio na mustakabali. Tufahamu kwamba vita viko mbele yetu kama jamii za Mlima Kenya. Tusikubali kuogopeshwa na wasiotutaka kuona tukidumisha umoja wetu,” akasema Mzee wa Njoka.

Naye Bw George Maara, ambaye ni mwanasiasa wa Kiambu, alisisitiza kinara wa siasa za Mlima Kenya ni Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

“Bw Kenyatta ndiye alipewa mamlaka ya kisiasa na kitamaduni kutuongoza. Akichoka na wadhifa huo ataturejeshea mamlaka hayo,” akasema Bw Mara.

Aidha Limuru III limeonekana ni kongamano la kuonyesha kutofurahishwa na sera za serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto na kusikitika kukataa kumsikiliza Bw Kenyatta aliyewataka wamchague Bw Raila Odinga wa Azimio La Umoja-One Kenya.

Washirikishi walisema kwamba mwaka 2027 watafanya maamuzi ya kumchagua kiongozi anayejali kikamilifu maslahi ya watu wa Mlimani na kwamba serikali iliyoko mamlakani sasa isipojirekebisha, itaangushwa katika uchaguzi mkuu.

Bw Kioni alidai kulikuwa kumepangwa njama ya kutibua Limuru III lakini “vijana wetu wakavuruga na kusambaratisha njama hiyo”.

“Utawala wa sasa umefanya maisha ya Wakenya kuwa magumu,” akasema Bw Kioni.

Bw Kioni aliongoza harambee ya kuchangisha pesa ili kusaidia watu waliokamatwa Naivasha katika mzozo wa ardhi na kampuni inayohusishwa na Rais Ruto.

“Serikali ina kanuni kali za kutoza ushuru na kutoheshimu maslahi ya Mlima Kenya,” akasema.

Kongamano hilo lilivutia wabunge watatu ambao ni Mbunge wa Embakasi Magharibi Mark Mwenje (Jubilee) , Mbunge wa Starehe Amos Mwago (Jubilee) na Mbunge wa Githunguri Gathoni wa Muchomba.

Kiongozi wa walio wachache katika bunge la kaunti ya Kiambu Ken Odhiambo ambaye pia ni diwani (MCA) wa Kahawa Sukari, alishutumu utawala wa Dkt Ruto kwa kutofanya jitihada zozote za kujihakikishia kuwa haukuwekwa madarakani kwa njia ya udanganyifu katika uchaguzi.

Katibu Mkuu wa muungano wa kitaifa wa madiwani Bw Stanley Karanja alisema Mlima Kenya wanajuta kwa sababu “hata nyadhifa hizo kuu zinazoshikiliwa na watu wetu wa Mlima Kenya katika serikali ya Dkt Ruto zimeishia kuwa za kuendeleza usaliti dhidi ya watu wetu”.