Jamvi La Siasa

Maandamano yalivyoanika jinsi ‘ndoa’ baina ya Ruto na Gachagua inavyoyumba

Na BENSON MATHEKA June 29th, 2024 3 min read

MZOZO kati ya Rais William Ruto na Naibu wake Rigathi Gachagua ulianikwa wazi kufuatia misimamo yao tofauti kuhusu jinsi serikali ilivyoshughulikia maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024.

Tofauti na siku za mwanzo za utawala wa Kenya Kwanza ambapo viongozi hao walionekana kushauriana kuhusiana na masuala muhimu ya kitaifa, mnamo Jumatano wawili hao walihutubia taifa kila mmoja kivyake baada ya waandamanaji kuvamia Majengo ya Bunge.

Rais Ruto aliwakusanya wabunge wa Kenya Kwanza katika Ikulu ya Nairobi kutangaza kwamba hangeidhinisha mswada tata wa Fedha huku Gachagua akihutubia taifa kutoka Mombasa akionekana kuwa mpweke.

Kwa suala muhimu la kitaifa kama uasi dhidi ya serikali, ilitarajiwa rais na naibu wake wangehutubia taifa pamoja. Hata hivyo, iliibuka kuwa viongozi hao wawili wameacha kushauriana kuhusu masuala muhimu au hawakuwa wameshauriana kuhusu jinsi ya kukabili maandamano.

SOMA PIA: Hofu Rais Ruto anapigana vita vingi mno

Gachagua na wabunge wa upinzani wa Kenya Kwanza ambao walipiga kura dhidi ya mswada huo hawakuwa katika Ikulu Jumatano, ishara kwamba kuna mpasuko katika serikali.

“Hotuba zao zilikuwa tofauti sana. Huku Ruto akilegeza kamba kuhusu mswada huo ambao aliahidi kutotia saini, Gachagua alichagua ujumbe tofauti, akimlaumu Mkurugenzi Mkuu wa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS) Noordin Haji kwa yaliyotokea Jumanne,” asema mdadasi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.

Kulingana na mchambuzi huyo, kutoa hotuba tofauti ni ishara ya wazi kwamba hali sio shwari baina yao.

“Kwa kuwa rais na naibu wake walikuwa nchini, wangehutubia taifa pamoja. Kukosa kufanya hivi walianika tofauti zao kwa vitendo na kwa maudhui ya hotuba zao,” akasema Gichuki.

Wiki iliyopita, wawili hao waliungana na wabunge wa muungano tawala katika Ikulu wakati mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya Bunge la Kitaifa Kimani Kuria na Kiongozi wa Wengi Kimani Ichungw’a walitangaza uamuzi wa kuondoa baadhi ya hatua za ushuru zilizokuwa katika mswada wa fedha uliopingwa.

SOMA PIA: Kambi hasimu zajigawa ndani ya UDA ‘sawa na ilivyokuwa wakati wa Uhuruto’

Kiongozi wa nchi alipokuwa akieleza sababu zilizomfanya kusikiliza malalamishi ya waandamanaji na uamuzi wake wa kukataa kutia saini mswada huo kuwa sheria, Gachagua alimwaga hasira zake kwa Mkurugenzi wa Huduma ya Taifa ya Ujasusi Noordin Haji akimlaumu kwa kumpotosha rais.

Gachagua alimkashifu Bw Haji kwa kupanga njama ya kuchafua majina ya baadhi ya viongozi akiwemo yeye kwa kuwataja kama wafadhili wa maandamano.

Wachambuzi wa siasa wanasema kwamba kwa Gachagua kuchagua kutumia athari za maandamano dhidi ya Mswada wa Fedha, kuanika tofauti zake na rais, kuna uwezekano mojawapo wa sababu za uhusiano wao kuingia baridi ni masuala ya kifedha.

“Kuna uwezekano mkubwa kwamba mpasuko kati ya viongozi hao wawili unatokana na masuala ya bajeti na fedha. Kumbuka Gachagua amekuwa akisisitiza kuwa serikali ni sawa na kampuni ya wenyehisa na rais amekuwa akimpuuza akisisitiza kila sehemu ya nchi inastahili kupata maendeleo,” asema mchambuzi wa siasa Peter Ouma.

SOMA PIA: Msafara wa Rais Ruto waacha wabunge walioandamana naye kwa mataa Nyahururu

Ouma anahusisha tofauti hizi pia na masuala ya chama tawala ambapo mirengo imeibuka katika uchaguzi wa mashinani mmoja ukiwa wa Gachagua na mwingine ukiegemea rais.

“Kumekuwa na mirengo miwili katika uchaguzi wa UDA ishara kwamba kila mmoja anataka kudhibiti chama tawala na mvutano ukasababisha uchaguzi wa mashinani katika baadhi ya maeneo kuahirishwa,” akasema Ouma.

Wadadisi wanasema kwamba huenda kuungana kwa chama cha Amani National Congress (ANC) cha Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na UDA kuliongeza uhasama kati ya rais na naibu wake.

SOMA PIA: Mambo hayatakuwa rahisi, vijana wa Gen Z waonya Ruto, wabunge

“Kumekuwa na vita vya ubabe wa mamlaka kati ya Gachagua na Mudavadi na hatua ya ANC kumezwa na UDA kumemwacha naibu rais na washirika wake bila usemi katika chama tawala. Kwa ufupi, Gachagua amesukumwa nje ya serikali aliyosaidia kuunda na anatumia kila nafasi kama vile maandamano kuelezea hasira zake,” akasema Ouma.

Wiki chache zilizopita, Gachagua alionekana kulaumu ukuruba wa Rais na kiongozi wa ODM Raila Odinga kwa masaibu yake akisema kwa vile waziri mkuu huyo wa zamani alifanya eneo la Mlima Kenya lichukie rais mstaafu Uhuru Kenyatta, hakuona sababu ya kutoridhiana naye kwa kuwa Rais Ruto amemkumbatia Raila.