Makala

Sehemu ya mbele King Fahd Hospital yageuzwa makutano ya kupitisha muda

May 3rd, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

UMARIDADI wa sehemu ya mbele ya Hospitali Kuu ya Rufaa ya King Fahd kisiwani Lamu umewavutia wananchi wengi wakiwemo mahasla ambao wameligeuza eneo hilo kuwa makutano ya kupitisha muda.

Hali hiyo hata hivyo imelalamikiwa na baadhi ya wasimamizi wa hospitali hiyo wanaodai kuwa mahasla hao ni kero kwani wamekuwa wakishinda hapo huku wakipigia kelele zinazowafikia na kuwataabisha wagonjwa ndani ya hospitali.

Hospitali Kuu ya Rufaa ya King Fahd ndiyo kubwa zaidi kote Lamu, hivyo kuhudumia mamia ya wagonjwa kila siku.

Katika mahojiano na Taifa Leo mnamo Ijumaa, Waziri wa Afya na Mazingira wa Kaunti ya Lamu Dkt Mbarak Bahjaj, alisema licha ya eneo hilo kutengenezwa ili liwe baraka kwa hospitali na umma unaofika kutibiwa kwa ujumla, kwa sasa limegeuka kuwa la maudhi.

Mahasla, hasa wale waraibu wa miraa na muguka, wanalalamikiwa kwa kushinda kuketi kwenye sehemu hiyo wakitafuna miraa au muguka huku wakipiga gumzo kwa sauti ya juu.

Kuna wale wanaokashifiwa kwa kutumia lugha chafu au ile ya matusi wakati wakibarizi eneo hilo huku wakitafuna miraa au muguka bila kujali kwamba eneo hilo linafaa kupewa heshima au taadhima yake.

Dkt Bahjaj alisema imefikia wakati ambapo ikiendelea hivyo huenda serikali ya kaunti ikalazimika kutumia polisi kuwafurusha kwa nguvu wale wanaojikusanya pale na kupiga gumzo zisizofaa.

“Hali kwa sasa ni mbaya. Haituridhishi kamwe. Wanaofika sehemu ya mbele ya King Fahd Hospital kubarizi sasa wamegeuka kuwa kero. Tumeongea nao mara kadhaa wabadili tabia zao lakini ni wagumu. Ikilazimu pengine tutawapelekea polisi pale wafurushwe,” akasema Dkt Bahjaj.

Mbali na umaridadi ambao tayari umefanyiwa sehemu hiyo ya mbele ya King Fahd Hospital, serikali ya kaunti ya Lamu kwa ushirikiano na wadau, ikiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi, UN-Habitat, wana mpango wa kulifanyia uboreshaji zaidi eneo hilo hivi karibu.

Mradi huo unakadiriwa kwamba utatumia kima cha Sh50 milioni.

Waziri wa Afya na Mazingira wa Kaunti ya Lamu, Dkt Mbarak Bahjaj. Anasema wanaobarizi kwenye sehemu ya mbele ya hospitali ya King Fahd kisiwani Lamu wamegeuka kuwa kero kwa sababu wanapiga kelele. PICHA | KALUME KAZUNGU

Dkt Bahjaj alisema kuna mpango wa kufunga maeneo ya kuingilia sehemu hiyo hivi karibuni.

“Kupitia UN-Habitat, twataka eneo hilo zima lifanyiwe uboreshaji ili liwe sehemu kamili ya kujivinjari, japo kwa mpangilio kinyume na sasa. Mradi huo unapaswa kuanza wakati wowote kuanzia sasa. Punde utakapoanza, hakuna mtu ataruhusiwa kuingia ovyoovyo isipokuwa wagonjwa watakaobebwa kwa tuktuk ambulensi maalum. Mradi utakamilishwa kufikia Desemba mwaka huu,” akasema Dkt Bahjaj.

Baadhi ya wakazi, ikiwemo mahasla waliohojiwa na Taifa Leo, aidha walikuwa na hisia mseto kuhusiana na lalama hizo.

Simon Mwangi alisema sio mahasla wote wanaofika eneo hilo la hospitali ya King Fahd ambao huleta kero zinazodaiwa.

“Sio wote ni wasumbufu. Ni baadhi tu ya watu… hasa hawa wanaokuja hapa kutafuna miraa. Hao ndio ambao hawazungumzi kwa sauti ya chini,” akasema Bw Mwangi.

Aliongeza kuwa maneno ya ‘wachanaji miraa’ huwa makali.

“Iwapo wataamua kutufurusha basi ni watukague kwanza ili kujua ni yupi hana tatizo na wale wenye balaa waondolewe. Tumependa mahali hapa. Ndio sehemu bora ya kupunga upepo wa bahari,” akaongeza.

Bi Swabra Omar alipongeza hatua ya kaunti kutaka wanaopoteza muda wao wakirandaranda na hata kupigia kelele wagonjwa kwenye sehemu hiyo ya mbele ya hospitali ya King Fahd waondolewe mara moja.

Sehemu ya Huduma za Dharura kwenye hospitali ya King Fahd kisiwani Lamu. Mahasla wanaopiga kelele nje ya hospitali hiyo ni kero kwa wagonjwa. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bi Omar alisema kuondoa watu wengine na kuacha baadhi yao kutaleta mgawanyiko na malalamiko mengi.

“Mimi mwenyewe ni shahidi kuwasikia hawa watu wakipiga kelele nje ya hospitali wakati niko na mgonjwa wangu hospitalini. Hakuna wa kuhurumia hapa. Kisiwa cha Lamu kina maeneo mengi ya watu kubarizi. Si lazima mbele ya hospitali ambapo mwishowe wagonjwa wanakoseshwa mapumziko yafaayo na amani yao,” akasema Bi Omar.

Bw Yusuf Abdalla aliwasihi wananchi kuheshimu eneo la hospitali na pia kutii maamuzi yote kaunti itachukua kuhusiana na suala hilo.

Pia aliwataka wakazi kutambua kuwa Lamu ni kubwa.

“Tuko na fukwe za bahari, hoteli za kuelea ndani au katikati ya bahari, milima ya mchanga mweupe kule Shela, matumbawe ya kuondoa msongo wa mawazo kule Mkanda. Kwa nini watu wapiganie tu eneo moja dogo kama lile la mbele ya King Fahd Hospital eti kwa kigezo cha kutaka kubarizi? Tukome kusumbua,” akasema Bw Abdalla.

Hospitali Kuu ya Rufaa ya King Fahd ina karibu miaka 40 sasa.

Ilianzishwa miaka ya themanini (1980s), wakati huo ikitambulika kama Hospitali Kuu ya Wilaya ya Lamu.

Mnamo mwaka 1984, Ufalme wa nchini Saudi Arabia, kupitia mfalme wake kwa wakati huo, King Fahd Ibn Abdul Aziz Al-Saud, ilitunuku jamii ya Lamu zaidi ya Sh100 milioni ili kutekelezea mradi wa ujenzi wa hospitali.

Fedha hizo zilitumika kuijenga upya na kuipanua hospitali Kuu ya Wilaya kisiwani Lamu.

Baada ya kukamilika kwake mnamo 1989, wakazi wa Lamu, kama mojawapo ya hatua ya kumuenzi mfalme huyo wa Saudi Arabia, wakaibandika hospitali hiyo jina King Fahd ambalo limedumu hadi leo.