Makala

TUONGEE KIUME: Kohoa kama mume, usiumie kimya kimya, usikubali kusukumwa

Na BENSON MATHEKA June 24th, 2024 2 min read

MBONA kaka wananyamaza wakisumbuliwa na wake wanaopenda kugombana bila kusema changamoto ni nini na wanatarajia wanaume waitambue.

Mbona? Basi akina dada zindukeni. Chali akitulia ukiwa msumbufu kwake kwa kila aina, iwe ni kumshinikiza kufanya mambo asiyopenda au asiyoweza unamuua kimya kimya.

Ukiendelea kumsumbua mwanamume bila kusema shida ni nini, utang’oa mapenzi aliyonayo kwako kutoka moyoni mwake na mwenye hekima, atanyamaza akivumilia na kuumia.

Huu ndio ukweli wa mambo; wanawake wengi ni walalamikaji wazuri bila vitendo. Ni wazuri sana katika kulalamika bila kuleta suluhu wala kufanya lolote kuhusu kile wanacholalamikia na kwa kufanya hivi, wanatesa wachumba wao.

Ukiendelea kufanya hivi kwa mumeo, hatakuchukulia kwa uzito. Kuna hili ambalo wanaume wanakwama nalo bila kuwaambia wanawake; kwamba ni muhali kuchukia mama yao.

Dada, ikiwa haupendi mama ya mumeo, tayari unafanya kukupenda kuwa vigumu kwake. Unahitaji kuelewa kwamba kila mtu anapenda mama yake, na wewe haushindani na  mama ya mumeo. Usipande mbegu ya chuki kati ya mumeo na mama yake, unaalika laana katika ndoa yako.

Mama ya mumeo akiwa mbaya kwako, tumia hekima uishi naye, mumeo hawezi kuwa na mama mwingine jinsi wewe hauwezi kuwa na mama mwingine. Kaka, usichukie mama yako au uache kumsaidia kwa sababu anakosana na mkeo. Kohoa, nguruma kama simba, wika kama jogoo.

Sumu nyingine ambayo inafanya akina kaka kusinyika na wake zao na kuwatoa moyoni kimya kimya ni kulinganishwa na wanaume wengine. Hii ni balaa kubwa ambayo mwanamume anapovumilia, inamuua kimya kimya.

Ukienda nyumbani kwa rafiki yako na uone gari jipya ambalo mumewe amemnunulia ukifika nyumbani, usianze kumdhulumu mumeo kumtaka akufanyie vivyo uwe kama  huyo shoga yako. Kuvumilia mwanamke  mwenye tabia hii, kumepeleka wanaume kaburini kimyakimya.

Kaka, mwanadada anayesahahu ghafla unachoweza kumudu akiiga wengine licha ya wewe kujitolea na kutumia uwezo wako kwake anakusindikiza kaburini pole pole.

Jambo moja ambalo wanaume huchukia ni mkewe kumwambia “wenzako wako ni hivi na hivi, mbona wewe.”

Heshima ni hitaji kuu la kwanza la kila mwanaume. Heshima ni kama oksijeni  kwa uhusiano wa mapenzi na ndoa. Kwa hili, mume hataki mke anayemkatiza akizungumza. Mwanamume hupenda mke anayemsikiliza kwa kwa makini na kutoa maoni au majibu akimaliza kumwaga yaliyo moyoni mwake.

Unapojifanya kuwa mwanafunzi wa mumeo kwa kuelewa anachotaka na asichokipenda na kukitenda, unajihakikishia furaha na upendo na unampa uhai wa kujenga ndoa yenu, kufanya kinyume ni kuiua.

Mwanamume hawezi kuchoshwa na mwanamke anayemwamini. Mke anayemwamini mume hawezi kuwa msumbufu, hamlinganishi na wanaume wengine, anaheshimu mama yake. Ndivyo walivyo wanaume. Dada, utakosea sana ukudhani kulisha mume asali akoleze ndicho anachotarajia kutoka kwako.