Michezo

Uingereza yafuzu kwa robo fainali za Euro 2024 kimuujiza

July 1st, 2024 2 min read

NYOTA Jude Bellingham alikuwa mwokozi wa Uingereza mnamo Jumapili usiku timu hiyo ikikodolea macho kubanduliwa Kombe la Ulaya (Euro) 2024, alipofunga bao dakika ya 90+5 kuanza ufufuo ulioishia katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Slovakia na hivyo kuzoa tiketi ya robo-fainali.

Katika mechi ambayo kwa mara nyingine Uingereza – maarufu Three Lions – walikuwa zegezege, kinda huyo mwenye umri wa miaka 21 alitinga bao la aina yake la mtindo wa bycicle kick dakika za nyongeza kusawazisha dhidi ya Slovakia – waliotangulia kufunga bao dakika ya 25 kupitia Ivan Schranz.

Ikalazimu mechi kuchezwa muda wa ziada ili kuamua mshindi.

Ni hapo ambapo nahodha na straika Harry Kane alitinga goli la ushindi dakika ya 91, kuhakikisha kocha Gareth Southgate na kikosi chake kinasonga mbele hatua ya 8-bora nchini Ujerumani.

Licha ya ushindi huo Southgate atalazimika kufanya muujiza kuleta msisimko uwanjani kwani mashabiki wa Uingereza kwa mara nyingine walilalamikia ubutu wa timu yake ambao umewaseta katika kipute hicho tangu mwanzoni.

Bellingham amekuwa katika fomu nzuri kwa klabu yake ya Real Madrid kwenye Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na inaonekana atazidi kuwa tegemeo kuu kwa timu yake watakapo menyana na Uswisi siku ya Jumamosi katika robo-fainali.

Akizungumza baada ya ushindi wao, Bellingham aliondolea mashabiki hofu.

“Nina furaha sana. Ushindi mzuri, tena tumefuzu raundi nyingine. Gemu yetu ilikuwa nzuri, na tutafanya vyema hata zaidi katika mechi zilizosalia. Tulidhibiti mpira pakubwa na kufanya mashambulizi, labda tu kukosa kufunga,” alieleza.

Akaongeza: “Tumeshinda pamoja. Sio mimi, sio Harry, sio mtu binafsi; ni wachezaji kama Ivan Toney, Eberechi Eze, Cole Palmer na Bukayo Saka. Ni kujitolea kwa ajili ya timu, na hilo ndilo tunahitaji.”

Jumanne ni Romania vs Uholanzi na Austria vs Uturuki

Nahodha wa Uholanzi, Virgil van Dijk, ameonya wenzake kuwa makini watakapokabiliana na Romania katika uwanja wa Munich leo usiku kusaka tiieti ya robo fainali ya Euro 2024.

Uholanzi walifuzu kwa hatua ya 16-bora kwa kuwa miongoni mwa timu bora zilizomaliza katika nafasi ya tatu na alama zao nne.

Ilianza dimba kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Poland, ikatoka sare 0-0 na Ufaransa kabla kupepetwa 3-2 na Austria mechi ya mwisho.

“Timu haijafanya vyema kama tulivyotarajia. Lazima turekebishe makosa kabla mechi hiyo (ya leo).”

Huu utakuwa ni mchuano wa pili wa Euro kukutanisha Romania na Uholanzi.

Uholanzi iliibuka kidedea 2-0 katika hatua ya makundi makala ya 2008.

Aidha, katika michuano 14 iliyopita kwenye mashindano yote ambayo wamekabiliana na Uholanzi, Romania imeshinda moja peke, ikasare tatu na kulambishwa sakafu mara 10.

Mbovu zaidi imefunga magoli matatu pekee na kutoa ndani 29.

Isitoshe, Romania imekomolewa katika mechi nne zilizopita mfululizo.

Nayo Austria itakabana koo na Uturuki katika uwanja wa Red Bull Arena jijini Leipzig katika mechi ya pili ya leo.

Austria ilishinda 6-1 timu hizi zilipokutana katika mechi ya kirafiki mwezi Machi mwaka huu.

In competitive matches, Türkiye are unbeaten in their last five games against Austria (W4 D1), keeping a clean sheet each time; this is the first such meeting since a goalless draw in a EURO 2012 qualifier in September 2011.

Hata hivyo, katika mechi za ushindani Uturuki haijapoteza katika mechi tano zilizopita – imeshinda nne na kutoka sare moja.

RATIBA YA JUMANNE:

Romania vs Uholanzi (7:00pm)

Austria vs Uturuki (10:00pm)