Makala

Vituo vipya vya afya mashinani vyasifiwa kupunguza vifo vya mama na watoto

Na OSCAR KAKAI July 4th, 2024 2 min read

KWA muda mrefu, wakazi mashinani katika kaunti ya Pokot Magharibi wamekuwa wakitegemea kambi za afya ama mitishamba kama matibabu.

Wakazi wengi ambao huwa wagonjwa huamua kuuza mifugo wao ili waweze kupata matibabu.

Hii ni kutokana na uhaba wa vituo vya afya katika maeneo ya mashinani suala ambalo limekuwa mzigo mkubwa kwa wakazi.

Vituo vya afya viko mbali suala ambalo huchangia akina mama kujifungulia nyumbani kutokana na kuchelewa kufika hospitalini.

Hii huchangia vifo vingi vya watoto na akina mama wajawazito wakati wa kujifungua.

Hata hivyo, wakazi katika vijiji kadhaa vya mashinani katika wadi ya Chepareria wana kila la kutabasamu badaa ya kufunguliwa kwa vituo vya afya.

Kati ya vituo vipya vya afya ni wadi ya wagonjwa ya Chepareria, zahanati za Senetwo na Propoi ambazo zinalenga kupeleka huduma za afya karibu na wakazi.

Kulingana na wakazi, historkia imewekwa sababu wamekuwa wakitembea zaidi ya kilomita ishirini kupata vituo vya afya.

Wakazi hao wamekaribisha vituo hivyo wakiitaka serikali kutuma wahudumu wengi wa afya ili kusaidia wakazi.

Rosemary Tulel, mkazi alipongeza hatua ya ujenzi wa vituo hivyo akikumbuka changamoto za awali kufikia vituo vya afya.

“Vituo hivi vya afya vitasaidia akina mama kujifungua vyema na afya kuimarika,” alisema.

Alisema kuwa wanawake wengi wamepoteza watoto wakati wa dharura na suala hilo sasa litafikia kikomo sababu vituo vya afya vimefunguliwa.

“Sasa shida zetu zimepungua, tunashukuru serikali ya kaunti,” alisema.

Bi Tulel alisema kuwa wamekuwa na shida nyingi sababu eneo hilo lina magojngwa mengi ya  malaria, homa ya matumbo, Brucella na mengine yanayosababishwa na maji.

“Tumeumia kwa muda mrefu kukosa nauli ya kufika kwenye kliniki na sisi huamua kujifungulia nyumbani. Hatutaenda tena katika hospitali ya kaunti ndogo ya Chepareria kupokea matibabu. Vituo hivyo vinatuokoa pakubwa,” alisema.

Mkazi Yolekirisi Losili kutoka eneo la Ywalateke alisema, “Wadi ya akina mama kujifungua inaokoa maisha na kupungua wakazi kusafiri hadi hospitali ya rufaa ya Kapenguria.”

Naibu wa Chifu wa kata ya Ywalateke, Japheth Ruto alisisitiza kuwa kituo hicho kitabuni ajira kwa wakazi.