Makala

Aukot aomba mahakama itangaze wakuu serikalini hawafai kushikilia vyeo

May 19th, 2024 4 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu sasa imeombwa itangaze kwamba Rais William Ruto, mawaziri wawili na Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome hawafai kuhudumu katika nyadhifa zao kwa kukandamiza Katiba na kukaidi maagizo ya korti kwamba maafisa wa polisi wapatao 1,000 wasipelekwe Haiti.

Mbali na Rais Ruto, mahakama imeombwa iwang’atue kazini mawaziri Kithure Kindiki (Usalama wa Ndani) na Musalia Mudavadi (Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigeni) kwa kuvunja sheria na kupuuza maagizo ya mahakama sawia na kukandamiza Katiba.

Ijapokuwa ombi hili limewasilishwa, Sheria inasema kwamba Rais anayehudumu hafai kushtakiwa ama kwa kesi ya uhalifu ama kesi yoyote nyingine ile isipokuwa kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa kiti cha urais.

Jaji Enock Mwita aliyesikiliza kesi ya kupinga polisi kupelekwa nchini Haiti alikuwa ameondoa jina la Dkt Ruto kuwa miongoni mwa washtakiwa.

Ombi hili la kutaka Rais na mawaziri Kindiki na Mudavadi, pamoja na Bw Koome kutangazwa hawafai kuhudumia umma liliwasilishwa kortini na Dkt Ekuru Aukot, Miruru Waweru na chama cha kisiasa cha Thirdway Alliance Kenya.

Kesi hiyo iliwasilishwa na wakili Charles Midenga anayesema mnamo Januari 26,2024 Jaji Mwita alifutilia mbali agizo maafisa wa polisi wapatao 1,000 wasipelekwe kudumisha amani nchini Haiti.

Jaji Mwita alisema sheria ya Kenya inaruhusu tu maafisa wa vikosi vya ulinzi yaani Jeshi la Nchi kavu, maafisa wa Jeshi la Wanahewa na maafisa wa Jeshi la Wanamajaji ndio wanaoruhusiwa kutumwa kudumisha amani mataifa ya ng’ambo yanayaogumbikwa na vurugu.

Jaji huyo alizima hatua ya kuwapeleka maafisa wa polisi akisema “uamuzi huo unakinzana na sheria.”

Washtakiwa hao watatu, Bw Midenga anasema, wamekaidi agizo la mahakama na kwamba kikosi cha kwanza cha maafisa wa polisi kinatazamiwa kuondoka nchini Machi 23, 2024, kusafiri hadi Haiti.

Bw Midenga alieleza kwamba Haiti haina mkataba wowote na Kenya wa kubadilishana vikosi vya usalama kwa mujibu wa Sheria nambari XIV na Sehemu nambari 107 na 108 za Sheria za kudhibiti Kikosi cha Polisi.

Mahakama ilielezwa Haiti haijawasilisha ombi rasmi Kenya kwamba inahitaji polisi kuhudumu nchini humo.

Mahakama Kuu ilielezwa hakuna Serikali rasmi nchini Haiti. Pia hakuna Bunge ambalo linaweza kutunga na kupitisha sheria polisi wa Kenya wapelekwe kule.

“Vitendo vya Rais Ruto, Prof Kindiki, Bw Mudavadi na Bw Koome vinadharau katiba na maagizo ya mahakama,” Bw Midenga alisema katika cheti cha dharura alichoandamanisha kesi hiyo.

Dkt Aukot alikuwa ameshtaki Baraza la Kitaifa la Usalama, Inspekta Jenerali, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, Wizara ya Usalama wa Ndani na Mwanasheria Mkuu.

“Endapo mahakama hii haitaingilia na kuwazima washtakiwa, polisi watapelekwa Haiti ambapo usalama wao hauna uhakika,” Bw Midenga akasema.

Bw Midenga anaomba kesi hiyo iratibiwe kuwa ya dharura.

“Naomba hii mahakama iwatangaze Rais Ruto, Bw Mudavadi, Prof Kindiki na Bw Koome, ambao ni watumishi wa umma, kwamba wamekandamiza Katiba na hawafai kuhudumu katika nyadhifa zao,” alirai Bw Midenga.

Pia aliomba wanne hao waagizwe wafike kortini kueleza sababu mbona wasisukumwe ndani miezi sita kwa kudharau maagizo ya mahakama na kukandamiza Katiba.

Bw Midenga aliomba kabla ya ombi la kutangazwa kwa wanne hao hawafai kuhudumu katika nyadhifa zao, watii agizo la kutowapeleka polisi Haiti.

Mnamo Januari 26, 2024, Serikali ilizimwa kupeleka maafisa 1,000 katika nchi ya Haiti.

Jaji Mwita alisema katika uamuzi wake kwamba Baraza la Usalama la Kitaifa (NSC) haina mamlaka yoyote kuamuru kupelekwa kwa polisi nchi ya Haiti.

Jaji Mwita alisema uamuzi wa Rais Ruto na wanachama wa baraza la NSC kuwapeleka maafisa wa polisi Haiti inakinzana na Kifungu nambari 240 (8) cha Katiba ya Kenya.

Kwa mujibu wa kifungu hiki maafisa wa polisi hawapaswi kupelekwa nchi za ng’ambo kudumisha amani.

Jukumu la kudumisha amani mataifa ya kigeni ni la Maafisa wa Jeshi.

Alisema sheria imeeleza kwamba maafisa wa Jeshi wanajumuisha Jeshi la Nchi Kavu, Jeshi la Angani (Airforce) na Jeshi la Wanamaji (Navy).

“Baraza la NSC halina mamlaka yoyote kuamuru maafisa wa polisi 1,000 wapelekwe Haiti kupambana na magenge yanayohatarisha maisha ya wananchi kule. Polisi si wanajeshi. Sheria inakitambua kikosi cha polisi kuwa cha kutoa huduma tu kwa wananchi humu nchini,” alisema Jaji Mwita.

Jaji huyo alisema ijapokuwa Rais Ruto aliahidi Baraza la Usalama la Umoja wa Kimataifa (UNSC) sheria za nchi hazitambui idara ya polisi kama “kikosi cha jeshi kilicho na uwezo kupelekwa kudumisha amani ng’ambo.”

Jaji huyo alisema polisi wameruhusiwa tu kudumisha usalama nchini tu na wala sio nje.

Ijapokuwa kauli mbiu ya kikosi cha polisi ni utumishi kwa wote, Jaji Mwita alisema “huduma za polisi zinapasa kutolewa humu nchini tu na sio ng’ambo.”

Alisema nchi ya Kenya na Haiti hazina mkataba wowote wa kubadilishana huduma za kiusalama na hivyo “basi Polisi wa Kenya hawawezi kuhudumu Haiti.”

Jaji huyo alisema iwapo kuna dharura humu nchini, baraza la usalama hutoa mwelekeo wa kuwapeleka maafisa wa polisi katika eneo husika na “mamlaka ya NSC hufika hapo tu.”

Hata wakati maafisa wa Jeshi wanapopelekwa nje, baraza la mawaziri hukutana na kupitisha idadi itakayoenda kisha hoja huwasilishwa Bungeni waende.

Baadaye Bunge huidhinisha wanajeshi waende, ndipo Mkuu wa Majeshi nchini (CDF) huteua wanajeshi na maafisa watakaosafiri kisha wanapewa bendera ya Kenya kupeperusha katika nchi wanakoenda kudumisha amani.

Jaji Mwita alisema ijapokuwa Waziri wa Usalama Prof Kindiki alipeleka suala la maafisa hao 1,000 wa polisi kuenda Haiti kujadiliwa Bungeni, hatua hiyo inakinzana na sheria.

“Baada ya kutathmini ushahidi wote uliowasilishwa mbele yangu, nimefikia uamuzi kwamba hatua ya NSC kupeleka polisi 1,000 Haiti inakinzana na Kifungu nambari 240 (8) cha Katiba. Polisi wa Kenya hawatapelekwa Haiti. Itakuwa ni kinyume cha sheria,” alisema Jaji Mwita.

Jaji huyo alisema kesi iliyowasilishwa na chama cha kisiasa cha Thirdway Alliance na Dkt Ekuru Aukot ya kupinga polisi wasipelekwe Haito iko na mashiko ya kisheria na inafaa kukubaliwa.