Makala

Wapigambizi tapeli watoweka na Sh20,000 familia ikitafuta mwili wa mama kwa wiki tatu

May 21st, 2024 2 min read

KASSIM ADINASI NA LABAAN SHABAAN

KAMA Irene Apondi, 56, angejua ziara yake shambani mwake mnamo Mei 3, ingemkutanisha na mauti, angeamua kukaa nyumbani.

Asubuhi hiyo, Bi Apondi alitoka nyumbani Sigweng Karuoth kuenda shambani karibu na ukingo wa River Nzoia katika kaunti ndogo ya Ugenya, Kaunti ya Siaya.

Mumewe alipoamua kuenda kumwangalia shambani, alizokuta ni nguo zake tu.

Ukaribu wa nguo zake mtoni ulifanya familia iamini pengine alianguka katika Mto Nzoia uliokuwa umejaa pomoni.

“Tulipanga kuhudhuria mazishi siku hiyo lakini aliamua kufika shambani kwanza,” alisema Bw Thomas Konyango ambaye ni mumewe.

Alipogundua amechelewa kurudi, ilibidi aende kumwangalia.

“Yeye ni mwanachama wa shirika la Mothers’ Union na akiwa pamoja na wengine, walikuwa wamepangiwa shughuli katika mazishi hayo. Wenzake walijaribu kumpigia lakini simu yake haikuingia kwa hivyo nikaamua kwenda kumtafuta,” mumewe alisimulia.

Bw Konyango alikuta mavazi ya mke wake yamekunjwa vizuri kando ya mto.

“Hatujui kilichofanyika lakini kama familia tunashuku aliamua kuoga na pengine aliteleza na kutumbukia mtoni na kusombwa na maji,” aliongeza na tangu Mei 3, familia bado inamtafuta.

“Kwa zaidi ya majuma mawili tumekuwa tukipiga kambi hapa tukimtafuta bila mafanikio. Tumefuata mto hadi Port Victoria ambapo mto humwaga maji lakini hatujafanikiwa,” anasema.

Familia hii imetumia hela nyingi kutafuta mwili wa Bi Apondi. Kulingana na Bw Konyango, wamelazimika kutumia boti za injini kutafuta mwili huo.

 “Tunalipa wapiga mbizi angalau Sh2,000 kila siku na kukodi boti. Tunalipa takriban Sh11,000 kila siku,” alisema Bi Elida Aloo, dadake marehemu.

Katika hali hii ngumu, familia imekutana na watapeli wanaowaibia pesa.

 “Watu wanakuja wakiwa na nia tofauti. Baadhi yao wanadai kuwa wana ujuzi na maarifa ya kuopoa mwili kutoka mtoni kwa muda mfupi. Kuna mpigambizi aliyekuja tukamlipa Sh20,000 na akatoweka,” alisema Frankline Odhiambo, jamaa ya marehemu.

Lakini familia imeshindwa kuendeleza operesheni kwa sababu ya kukosa pesa. Sasa wanaomba wahisani na serikali kuwapiga jeki.

“Tunataka sana kupata mwili wa mama yetu ili tumpe mazishi ya heshima,” anasema Miriam Otieno, bintiye marehemu.

Inadaiwa awali shughuli ya uopoaji iliendeshwa na maafisa wa majini wa Kenya Coast Guard lakini maafisa hao walibadili misheni baada ya maafisa wa polisi kuzama ziwani Victoria.

 “Ni makosa na si haki kusema kuwa polisi wamepuuza masaibu ya familia, tunahusika kikamilifu na matokeo yataonekana. Changamoto kuu ni mafuriko Mtoni Nzoia ambayo yanawapa wapigambizi changamoto,” akasema afisa wa Kenya Coast Guard aliyeomba asitajwe.