Siasa

Gachagua aambiwa mambo ni manne

May 24th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

ALIYEKUWA mbunge wa Gatanga Bw Nduati Ngugi amemshauri Naibu Rais Rigathi Gachagua kwamba ana mambo manne ya kujinusuru kutoka kwa kile alidai ni msukosuko wa kisiasa ambao unamkumba ndani ya serikali.

Kauli ya Bw Ngugi inajiri kukiwa na minong’ono kwamba ndoa ya kisiasa kati ya Rais William Ruto na Bw Gachagua inaingia mdudu.

Bw Ngugi alisema kwamba mambo hayo manne ni ama Bw Gachagua akae ngangari ndani ya serikali na apambane kimasomaso na misukosuko hiyo, amkabili Rais Ruto akimtaka awang’oe mamlakani waasi walio katika serikali kwa wito wa Bw Gachagua, atoke na aunde upinzani akilenga kuwania urais 2027, au akiwa tu ndani ya serikali, aungane na mrengo wa Azimio kumng’oa Rais Ruto 2027.

Wale ambao wandani wa Bw Gachagua wanadai wamemea pembe ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti Bw Ndindi Nyoro (Mbunge wa Kiharu), Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Bw Kimani Ichung’wah (Mbunge wa Kikuyu), Waziri wa Utumishi wa Umma Bw Moses Kuria na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Bi Anne Waiguru (Gavana wa Kirinyaga).

Wote wamenukuliwa katika visa na majukwaa mbalimbali ama kupitia wandani wao au wao wenyewe, wakiashiria kutomtambua Bw Gachagua na mamlaka yake pamoja na ufaafu wa kuwa mwaniaji mwenza wa Dkt Ruto mwaka 2027.

Bw Ngugi alisema kwamba kwa sasa Bw Gachagua ana bahati ya kuwa hata kuwe kumeharibika kiasi gani, Rais Ruto hawezi akamfuta kazi kwa kuwa kutazuka mgogoro wa kikatiba kwa kuwa tiketi yao ni moja.

“Kwa hivyo, Bw Gachagua ana hakikisho kwamba anaweza akadumu ofisini hadi 2027 lakini pia akiwa na ruhusa ya kujitoa kwa hiari,” alisema Bw Ngugi.

Hata hivyo, alimuonya kwamba kujiondoa ofisini kutampunguza makali kwa zaidi ya asilimia 80 kwa kuwa atapoteza cheo na mamlaka na pia mwanya wa kuunda mtandao wa kimataifa ambao husaidia katika uwaniaji wa urais.

Bw Ngugi alisema kwamba kwa sasa, sio siri kwamba Bw Gachagua anakumbwa na msukosuko mkuu wa kisiasa ambao unaonekana kusukwa kutoka kwa kona fulani serikalini huku baadhi ya wanasiasa wa Mlima Kenya wakitumiwa.

“Hata ikiwa Bw Gachagua anashikilia kwamba mambo yako sawasawa kati yake na mdosi wake, matamshi ya wandani wake kama Gavana wa Nyeri Bw Mutahi Kahiga yanaashiria kwamba hali si shwari kamwe,” alisema.

Bw Kahiga tayari ameteta kwamba licha ya serikali ya Kenya Kwanza kuundwa kwa asilimia 47 ya hisa za Mlima Kenya, kwa sasa kuna madharau ya wazi yanayoashiria njama kubwa ya kisiasa kusukwa kutoka nje ya Mlima Kenya.

Bw Kahiga alidai kwamba “njama hiyo inaonekana waziwazi kusukwa kutoka eneo la Rift Valley”. Hilo limeungwa na mbunge wa Embakasi Kaskazini Bw James Gakuya.

Bw Ngugi anasema kwamba “Bw Gachagua kwa kiwango kikuu alijihujumu kisiasa kupitia maongezi yake dhidi ya wadau wengi wa kisiasa nchini kiasi kwamba alijiangazia kama Naibu Rais wa Mlima Kenya wala sio wa kitaifa”.

Katika hali hiyo, Bw Ngugi alisema kwamba Bw Gachagua alijiangazia kama mshindani wa kisiasa wa wadogo wake wa Mlimani hivyo basi kujipata katika shida aliyo nayo kwa sasa.

Hata hivyo, Bw Ngugi alionya kwamba watu wa Mlima Kenya hawafai kushabikia masaibu ya Bw Gachagua kwa kuwa yatawaathiri moja kwa moja katika mikakati ya siasa za baadaye hasa za 2027 na 2032.

Alisema kwamba huu ni wakati wa jamii za kutoka Mlima Kenya kudumisha umoja na kushininikiza Bw Gachagua arekebishe pale huwa anakosea na ndipo eneo hilo liwe katika mkondo wa sauti moja katika chaguzi za 2027 na 2032.